Chanjo na kipimo cha Covid inahitajika kwa mashabiki wa Kombe la Afrika

Mashabiki watakaohudhuria mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi ujao nchini Cameroon watahitajika kuonyesha uthibitisho wa chanjo na kuwasilisha matokeo hasi ya kipimo cha UVIKO-19, maafisa walitangaza Alhamisi.

Tangazo hilo lilitolewa katika taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na mawaziri wa michezo na afya wa Cameroon pamoja na katibu mkuu wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), na inakuja wakati ambapo kuna tetesi kwamba michuano hiyo inaweza kufutwa au kuahirishwa tena.

“Mashabiki hawataweza kuingia viwanjani… isipokuwa wale waliochanjwa kikamilifu na kuonyesha kipimo cha PCR cha chini ya saa 72 au kipimo cha antijeni hasi cha chini ya saa 24,” waraka huo ulisema.

“Licha ya changamoto hii ya ziada inayoletwa na janga hili, Kombe letu la Mataifa lazima sasa lifanyike,” iliongeza.

Sherehe ya ufunguzi wa kinyang’anyiro hicho  inatazamiwa kufanyika katika Uwanja wa Olembe mjini Yaounde Januari 9 kabla ya mchezo wa kwanza kati ya wenyeji Cameroon na Burkina Faso. Fainali imepangwa kuchezwa katika uwanja huo mnamo Februari 6.