China Yazindua Kinywaji Chake Maarufu, Fenjiu Nchini Kenya

NAIROBI, Kenya- Wakenya wanaopenda bidhaa za Uchina sasa wana sababu ya kutabasamu baada ya Uchina kuzindua kinywaji chake cha kitamaduni maarufu kama Fenjiu Liquor katika hafla ya kufana jijini Nairobi Jumapili usiku.

Mvinyo huo maarufu wa Kichina, uliotengenezwa kwa mchele uliochomwa kwa zaidi ya miezi tisa na kuachwa kukomaa kwa miaka miwili, sasa unapatikana katika duka kubwa la China, duka la jumala la  Chinatown, iliyoko mkabala na Barabara ya Ngong jijini Nairobi.

Ni mara ya kwanza kwa kinywaji hicho chenye ladha tamu harufu ya kuvutia kupenya barani Afrika. Nusu lita huenda kwa KSh 2000-3000.

“Ni kinywaji kizuri sana, tuna imani kuwa Wakenya watakipenda,” Mkurugenzi wa duka ya jumla ya Chinatown, Mei Hong alisema.

“Pia tunaamini kuwa bei ni nzuri, lakini bado tunasoma soko la ndani ili kufanya marekebisho yanayofaa,” Hong alisema.

Hong alisema takriban masanduku 300-400 tayari yameingizwa nchini na yanapatikana katika duka kuu la Chinatown. Mipango tayari inaendelea kusambaza kinywaji hicho  cha hali ya juu katika maduka mengine ya ndani.

Kulingana na Hong, Kenya ni miongoni mwa masoko yaliyoimarika barani Afrika kwa bidhaa hiyo hivyo sababu ya kuwa ya kwanza barani humo kusambaza kinywaji hicho.

“Naipenda Kenya, nimeishi hapa kwa miaka 22, nina marafiki wengi wanaopenda bidhaa za China, hii ndiyo iliyotusukuma kuagiza pombe hii kutoka nje.

“Pia tuna Wachina wengi nchini Kenya na ni dhahiri wanakosa vinywaji kutoka kwa taifa lao kwa hivyo kulikuwa na haja ya kuagiza Fenjiu ili kuziba pengo hili,” alisisitiza.

Hong anaamini kuanzishwa kwa kinywaji hicho katika soko la Kenya pia kutasaidia kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo kati ya China na Kenya ambao tayari umedumu kwa miaka 60.

Idadi ya shughuli za Uwajibikaji kwa Jamii zimepangwa ili kusaidia kutangaza kinywaji hicho kuwa maarufu na kutoa ufahamu kuhusu bidhaa hiyo.

Fenjiu inatoka katika Mkoa wa Shanxi nchini China ambako imetengenezwa kwa maji ya asili ya visima vilivyopo kwenye Kijiji cha Apricot Blossom.

 Ni miongoni mwa vinywaji vitano vya kileo nchini China. Maudhui yake ya pombe ni kati ya 38% -60%.

Kinywaji hiki kinakumbukwa zaidi kwa kushinda medali ya dhahabu kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Panama mnamo 1916.

Mapema mwaka huu, China ilianzisha Bia ya Tsingtao katika soko la humu nchini ambalo pia linapendwa sana na Wachina, Wakenya na jamii zingine zinazoishi nchini.