Watu wanaotaka kukatisha maisha yao nchini Uswizi – mojawapo ya nchi chache zinazotoa ruksa kwa mtu kujitoa uhai- hivi karibuni wanaweza kupata njia mpya: chombo maalum kilichoundwa kwa mfumo wa 3-D ambacho muundaji wake anasema kinaweza kumaliza maisha ya mtu bila maumivu na kwa dakika chache tu.
Watu waliojitolea kukijaribu chombo hicho watashiriki kwenye majaribio yaliyopangwa kuanza mapema mwaka wa 2022, mtayarishaji wa chombo hicho, Philip Nitschke, aliiambia The Washington Post wiki hii.
Uchambuzi wa kisheria ulioidhinishwa na shirika lake lisilo la faida, Exit International, hivi majuzi ulihitimisha kuwa matumizi ya chombo hicho hayatakiuka sheria za kujitoa uhai za Uswizi, Nitschke alisema.
Kwa kubofya kitufe, chombo hicho hujaa gesi ya nitrojeni, ambayo hupunguza viwango vya oksijeni kwa haraka, na kusababisha mtumiaji wake kupoteza fahamu ndani ya dakika moja, Nitschke alisema. Mtu hapungukiwi na hewa wala kupata dhiki, alisema, lakini hufa kwa kukosa oksijeni baada ya kulala.
Kinadharia, chombo hicho kinaweza kupelekwa hadi pahali ambapo mtu angetaka kukatiza maisha yake alisema Nitschke, ambaye alielezea kuwa chombo hicho ni njia “maridadi” ya kufa.
“Chombo hicho kina muonekano mzuri na kinapendeza na ningependa watu wanaotaka kujitoa uhai wakitumie.”
Lakini tangu Nitschke azindue chombo hicho miaka minne iliyopita, amekabiliwa na viwango tofauti vya mshangao na laana, huku baadhi ya wakosoaji wakisema kuwa muonekano wa chombo hicho ni mojawapo ya matatizo yake makubwa.
Daniel Sulmasy, mkurugenzi wa Taasisi ya Maadili katika Chuo kikuu cha Georgetown, alisema muundo maridadi wa chombo hicho unaofanana na gari la kifahari “kunafanya kujitoa uhai kuonekana kama jambo la kupendeza.” Pia alisema anapinga mpango wa Nitschke kuchapisha maagizo ya kuunda chombo hicho mtandaoni, akibainisha kuwa inaweza kusababisha watu wengi zaidi kufa kwa njia hiyo.
Nitschke anasema kuwa chombo hicho ni salama na kitasaidia watu kufa bila kuhisi uchungu – na hatarajii jambo lolote la kushangaza wakati wa majaribio ambayo yatafanyika katika kliniki ya Uswizi. Takriban watu 12 watajitolea kukifanyia chombo hicho majaribio. “Tutastarehe baada ya kuwa na majaribio machache ya kwanza yenye mafanikio,” alisema.