Colombia: Takriban wafungwa 52 wafariki katika ghasia na moto gerezani

Jamaa wa wafungwa wavunja dirisha la gereza la Tulua, Idara ya Valle del Cauca, Colombia, Juni 28, 2022, baada ya wafungwa kadhaa kufariki kwenye ghasia walipochoma moto asubuhi na mapema kujaribu kuzuia polisi kuingia ndani ya jela lao.(Photo by AFP)

Takriban wafungwa 52 waliuawa na wengine 26 kujeruhiwa mapema Jumanne baada ya moto kuzuka wakati wa ghasia za magereza kusini magharibi mwa Colombia, shirika la magereza la kitaifa lilisema.

Mkasa huo ulitokea wakati wafungwa walipochoma moto mwendo wa saa 2:00 asubuhi, wakijaribu kuwazuia polisi kuingia kwenye kizuizi chao katika gereza la mji wa Tulua, alisema Tito Castellanos, mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Magereza (INPEC).

“Tumewatibu jumla ya majeruhi 26 na idadi ya vifo ni 52,” Cristina Lesmes, mkuu wa idara ya afya huko Valle del Cauca, alisema kwenye Twitter.

“Tuna watu katika hali mbaya sana na wana majeraha ya moto,” alisema.

Hapo awali Castellanos alisema idadi ya waliouawa kuwa 49 na wengine 30, wakiwemo walinzi sita wa magereza wakijeruhiwa na kuathiriwa na moto na moshi.”

Gereza hilo linalohifadhi wafungwa zaidi ya 1,200, lilikuwa limezingirwa na polisi na wanajeshi.

“Baada ya kutia moto magodoro, hawakuwa wamekadiria matokeo na kwa bahati mbaya hii ilifanyika,” Castellanos aliiambia Radio RCN.

Alisema moto huo umedhibitiwa na wazima moto.

Kufikia jioni, timu za uchunguzi zilikuwa zimeingia gerezani kujaribu kutambua miili.

Nje ya gereza, makumi ya wanafamilia walikusanyika wakitarajia kupata habari kuhusu wapendwa wao.

Afisa wa gereza alitoa orodha ya kwanza ya walionusurika.

“Sijui chochote, INPEC haitaturuhusu kuingia,” Maria Eugenia Rojas aliyetokwa na machozi, ambaye mwanawe Luis Miguel Rojas ni mfungwa katika jela ambako ghasia hizo zilitokea, aliambia televisheni ya Caracol.

Lorena, ambaye hakutaja jina lake la pili, aliambia gazeti la El Tiempo kwamba alikuwa amezungumza na mpenzi wake ambaye ni mfungwa mwendo wa alfajiri.

“Inaonekana kutokuwa na mantiki kwangu kwamba watu waliofungiwa ndani ya jengo wangechoma magodoro wakijua kuwa wangeweza kuungua,” alisema.

Hapo awali mamlaka ilikuwa imesema inachunguza iwapo kisa hicho kilitokea kama sehemu ya jaribio la kutoroka lakini baadaye walisema ni ghasia.

“Hali hii ilichochewa na mapigano yaliyozuka kati ya wafungwa. Mmoja wa wafungwa alichoma moto — alikuwa na hasira, hasira — kwa godoro, ambalo lilichochea moto,” Ruiz alisema.

Kulikuwa na wafungwa 180 katika sehemu ya gereza lililoathiriwa na moto huo.

Castellanos alipongeza juhudi za askari magereza kudhibiti moto huo na kuwasaidia kufikia salama.

Alisema iwapo hawangeingilia kati ‘matokeo yangekuwa mabaya zaidi.