Daraja lililojengwa kwa gharama ya Ksh 100M laporomoka

Daraja la Paai, Kaunti ya Kajiado

Daraja la mamilioni ya pesa lililojengwa na serikali ya kaunti ya Kajiado limeporomoka, wiki moja baada ya kuzinduliwa.

Daraja la Paai la lililogharimu takriban Ksh 100M liliunganisha kaunti ndogo tatu za Kajiado Mashariki, Kajiado Kusini na Kajiado ya Kati.

Wakaazi waliamka Alhamisi asubuhi na kupata daraja hilo limepinda katikati kufuatia mafuriko katika eneo hilo.

Wakati wa uzinduzi wake mnamo Februari 17, gavana wa Kajiado Joseph ole Lenku alisema uwekezaji huo mkubwa ulikusudiwa kuwezesha wakazi wa maeneo hayo kuvuka kutoka kijiji kimoja hadi kingine wakati wa msimu wa mvua.

Maeneo mengi ya nchi yameshuhudia mvua kubwa tangu Jumanne huku Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya ikionya kuwa mvua kubwa inatarajiwa katika maeneo ya nchi kati ya miezi ya Machi na Mei.

Katika taarifa rasmi, mtaalamu wa hali ya hewa alidokeza kuwa mvua nyingi itanyesha katika Bonde la Ziwa Victoria, Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa na Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa.

Shirika hilo pia lilisema kuwa mvua wastani itanyesha katika mikoa ya Kaskazini Mashariki na Pwani katika kipindi hicho.