Askofu Mkuu wa Afrika Kusini Desmond Tutu, alifariki Jumapili akiwa na umri wa miaka 90.
Tutu, ambaye kwa kiasi kikubwa alififia katika maisha ya umma katika miaka ya hivi karibuni, alikumbukwa kwa ucheshi na tabasamu lake — na zaidi ya yote mapambano yake dhidi ya dhuluma za kila namna.
Alikuwa Askofu wa Johannesburg kutoka 1985 hadi 1986 na kisha Askofu Mkuu wa Cape Town kutoka 1986 hadi 1996, katika hali zote mbili akiwa Mwafrika wa kwanza mweusi kushika nafasi hiyo.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, alipotangaza kifo cha askofu mkuu siku ya Jumapili, alimtaja kama mtu wa “akili ya ajabu, mwadilifu na alipinga ubaguzi wa rangi nchini humo.”
“Kufariki kwa Askofu Mkuu Desmond Tutu kunaashiria wakati mgumu kwa taifa letu baada ya kufariki kwa kizazi cha Waafrika Kusini mashuhuri ambao wametuachia urithi wa Afrika Kusini uliokombolewa,” alisema, wiki chache baada ya kifo cha FW de Klerk, rais wa mwisho mzungu wa nchi hiyo. Rais wa zamani wa Amerika Barack Obama, kiongozi wa kwanza mweusi nchini humo, alimsifu Tutu kama mtu mashuhuri na “aliyekuwa dira ya maadili kwa taifa hilo.”
“Askofu Mkuu Tutu alikuwa amejikita katika mapambano ya ukombozi wa waafrika kusini weusi katika nchi yake na pia alihusika na kupigani haki katika mataifa mengine duniani.” Obama alisema katika taarifa yake.
Waombolezaji walikusanyika katika parokia yake ya zamani huko Cape Town, Kanisa Kuu la St George, huku wengine wakikusanyika nyumbani kwake, wengine wakiwa na mashada ya maua, kulingana na AFP.
“Kama isingekuwa kwa mchango wake, pengine tungepotea kama nchi,” alisema Miriam Mokwadi, muuguzi mstaafu mwenye umri wa miaka 67.
Timu ya kriketi ya Afrika Kusini ilivaa vitambaa vyeusi mikononi kwa heshima yake katika siku ya kwanza ya mechi yao dhidi ya India iliyofanyika nchini Afrika Kusini.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema Tutu “alihimiza kizazi cha viongozi wa Afrika ambao walikubali mbinu zake zisizo za vurugu katika mapambano ya ukombozi.”
Viongozi wa Ulaya walitoa ujumbe wao huku Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akimtaja kama “mtu muhimu” katika mapambano ya kuunda Afrika Kusini mpya na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema Tutu “alijitolea maisha yake katika kupatikana kwa haki za binadamu na usawa.”
Vatican ilisema Papa Francis amehuzunishwa na kutoa “rambirambi za dhati kwa familia yake na wapendwa wake.”
Mwanaharakati wa miaka mingi, Tutu alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 1984 kwa kupambana na utawala wa wazungu wachache nchini mwake.
Alibuni neno “Rainbow Nation” kuelezea Afrika Kusini wakati Nelson Mandela alipokuwa rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo mnamo 1994.
Desmond Mpilo Tutu alipata mafunzo ya ualimu na kumuoa Nomalizo Leah Shenxane mwaka wa 1955, ambaye alipata naye watoto wanne.
Mnamo 1985, Tutu alikua Askofu wa Johannesburg na mnamo 1986 Askofu Mkuu wa Cape Town, wadhifa wa juu zaidi katika uongozi wa Anglikana kusini mwa Afrika. Katika nafasi hii alisisitiza mfano wa kujenga maelewano ya uongozi na kusimamia kuanzishwa kwa mapadre wa kike.
Tutu alistaafu mwaka wa 1996 na kuongoza safari ya kupata ukweli kama mkuu wa Tume ya Ukweli na Maridhiano, ambayo iliweka wazi maovu ya utawala wa kibaguzi. Hata hivyo, Tutu pia alikosoa chama tawala cha African National Congress (ANC) — chama kilichohusika pakubwa katika mapambano dhidi ya utawala wa wazungu wachache.
Tutu alimpinga Mandela kuhusu mishahara minono waliyokuwa wakilipwa mawaziri na kukosoa vikali ufisadi uliokithiri chini ya rais wa zamani Jacob Zuma.
Alitawazwa akiwa na umri wa miaka 30 na kuteuliwa kuwa askofu mkuu mwaka 1986, alitumia nafasi yake kutetea kuwekwa vikwazo vya kimataifa nchini humo ili kukomesha ubaguzi wa rangi, na baadaye alishawishi kupatikana kwa haki duniani kote.
Kuonekana kwake hadharani kulizidi kuwa haba na, mwaka huu alitoka hospitalini akiwa kwenye kiti cha magurudumu ili kupata chanjo dhidi ya UVIKO 19, alipunga mkono lakini hakutoa maoni.
Askofu mkuu alikuwa katika hali dhaifu kwa miezi kadhaa na alfariki mwendo wa saa 1:00 asubuhi (0500 GMT) siku ya Jumapili, kulingana na jamaa zake kadhaa waliohojiwa na AFP.
Wakfu wa Nelson Mandela ulimtaja Tutu kama “binadamu wa ajabu. Mwanafikra. Kiongozi. Mchungaji.”
Tutu alizaliwa katika mji mdogo wa Klerksdorp, magharibi mwa Johannesburg, mnamo Oktoba 7, 1931. Mzazi wake mmoja alkuwa mfanyakazi wa ndani na mwinhine mwalimu wa shule.
Alipata mafunzo ya ualimu kabla ya mfumo duni wa elimu uliowekwa kwa ajili ya watoto weusi kumchochea kuwa kasisi.
Aliishi kwa muda huko Uingereza, ambako, alipenda kuomba maelekezo ili tu aitwe “Bwana” na polisi wa kizungu.
Tutu alipinga bila kuchoka maswala kama vile ubaguzi wa rangi na dhulma dhidi ya mashoga.
Hakuhofia mwisho wake.
“Nimejitayarisha kwa kifo changu na nimesema wazi kwamba sitaki kuendelea kuwa hai kwa gharama yoyote,” alisema katika sehemu ya maoni katika gazeti la The Washington Post mwaka wa 2016.
“Natumai nitatunzwa na kuruhusiwa kumaliza safari ya maisha kwa njia niipendayo.”