Askari watatu wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na takriban waandamanaji 12 wameuawa katika maandamano ya kupinga Umoja wa Mataifa yanayoendelea mashariki mwa DR Congo, maafisa walisema Jumanne.
Hasira imechochewa na dhana kwamba MONUSCO, ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), unashindwa kufanya vya kutosha kukomesha mashambulizi ya makundi yenye silaha.
Umati wa watu siku ya Jumatatu ulivamia makao makuu ya MONUSCO na kituo cha ugavi huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, na maandamano hayo yakasambaa siku ya Jumanne hadi Beni na Butembo kaskazini.
Mkuu wa polisi wa Butembo Kanali Paul Ngoma alisema askari watatu wa kulinda amani, wawili wa India na Morocco – wameuawa na mwingine kujeruhiwa, wakati waandamanaji saba walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
MONUSCO ilisema Jumanne kwamba mwanajeshi mmoja na maafisa wawili wa polisi wa kijeshi wanaohudumu na Umoja wa Mataifa waliuawa katika shambulio kwenye kambi yake huko Butembo.
Mlinda amani mwingine alijeruhiwa vibaya sana.
“Washambuliaji walinyakua silaha kwa nguvu kutoka kwa maafisa wa Polisi wa Kitaifa wa Congo na kuwafyatulia risasi walinda amani wetu,” MONUSCO ilisema, na kuongeza kuwa ‘inalaani vikali’ shambulio hilo.
Jeshi la Morocco pia lilitoa taarifa na kuthibitisha kuwa askari mmoja wa kulinda amani wa Morocco ameuawa kwa kupigwa risasi, huku askari 20 kutoka kikosi cha MONUSCO cha nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika pia wakijeruhiwa wakati wa machafuko ya hivi karibuni.
Farhan Haq, msemaji wa Umoja wa Mataifa, aliwaonya waandishi wa habari mjini New York Marekani kwamba hali ni tete sana.
“Uimarishaji unahamasishwa,” alisema.
Katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa DRC Kinshasa, msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema kuwa takriban watu 15 wakiwemo askari watatu wa kulinda amani wameuawa katika machafuko ya hivi karibuni na watu 61 kujeruhiwa.
MONUSCO ni mojawapo ya operesheni kubwa zaidi za kulinda amani duniani.
Lakini imekuwa ikikosolewa mara kwa mara ambapo wengi wanaishutumu kwa kushindwa kufanya vya kutosha kumaliza umwagaji damu uliodumu kwa miongo kadhaa.
Zaidi ya makundi 120 yenye silaha yanazunguka katika eneo hilo lenye hali tete, ambapo mauaji ya raia ni jambo la kawaida na mizozo imesababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao.
Katika machafuko ya Jumatatu, mamia ya watu huko Goma walifunga barabara na kuimba nara za uhasama kabla ya kuvamia makao makuu ya MONUSCO na kituo cha usambazaji.
Waandamanaji walivunja madirisha na kupora vitu vya thamani, huku helikopta zikiwasafirisha kwa ndege wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kutoka katika majengo hayo na vikosi vya usalama vikifyatua vitoa machozi kwa nia ya kuwarudisha waandamanaji nyuma.
Vikosi vya usalama vya Congo vilizuia umati wa watu nje ya kituo hicho, ambao baadhi yao walikuwa na mabango yenye maandishi kama vile ‘Bye-bye, MONUSCO.”