Watu wanaoshukiwa kuwa waasi wamewaua raia kumi na wawili katika mashambulizi ya hivi majuzi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, maafisa wa eneo hilo walisema Alhamisi.
Daktari mkuu wa hospitali ya Oicha katika jimbo la Kivu Kaskazini alisema kuwa alipokea miili mitano siku ya Jumatano kutoka kwa kijiji kilichoko magharibi mwa mji huo.
Miili mingine saba iliwasili kutoka kijiji kingine magharibi mwa Oicha siku ya Alhamisi, daktari mkuu Jerome Munyambete alisema.
“Watu hawa waliuawa kwa mapanga na risasi,” alisema.
Darius Kasereka, mwakilishi wa mashirika ya kiraia huko Oicha, alithibitisha idadi ya waliouawa na kusema katika taarifa kwamba raia hao kumi na wawili waliuawa kikatili.
“Eneo linalozunguka Oicha limevamiwa na waasi wa ADF,” aliongeza, akimaanisha kundi la Allied Democratic Forces.
Kundi la ADF ni miongoni mwa wanamgambo wenye ghasia zaidi kati ya zaidi ya wanamgambo 120 ambao wanazurura mashariki mwa DRC.
Kundi hilo — ambalo kundi la Islamic State linadai kuwa tawi lake la kati mwa Afrika — limeshutumiwa kwa mauaji ya raia wa Congo pamoja na kufanya mashambulizi katika nchi jirani ya Uganda.
Rais wa Congo Felix Tshisekedi aliweka Kivu Kaskazini na jimbo jirani la Ituri chini ya usimamizi wa vikosi vya usalama mwaka jana katika jitihada za kukomesha ghasia.
Lakini hatua hiyo imeshindwa kukomesha mashambulizi dhidi ya raia.