DR Congo: Watu 26 wafariki baada ya kuangukiwa na nyaya za umeme

Watu 26 wamefariki baada ya kebo ya umeme kuanguka kwenye mtaro wa kupitishia maji sokoni katika mji mkuu wa Kinshasa DR Congo, mamlaka za mitaa zilisema.

“Kebo hiyo ilikatika na kuanguka kwenye mtaro uliokuwa umejaa maji baada ya mvua kunyesha asubuhi. Kwa sasa, watu 26 wamefariki kutokana na kupigwa na umeme,” Charles Mbutamuntu, msemaji wa serikali ya jimbo la Kinshasa, aliiambia AFP.

Mkasa huo wa Kinshasa ulitokea huku habari zikiibuka kuhusu mauaji ya watu wengi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo takriban watu 40 waliokimbia makazi yao waliuawa Jumanne jioni na wanamgambo waliokuwa na mapanga, kulingana na kundi la ufuatiliaji na vyanzo vya ndani.

Katika soko maarufu la chakula la Matadi-Kibala magharibi mwa Kinshasa,” watu wengi waliouawa walikuwa wafanyabiashara na wateja, na baadhi ya wapita njia,”Mbutamuntu alisema.

“Miili inapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na uchunguzi umeanza ili kubaini waliohusika na mauaji hayo.”

Ofisi ya Rais wa Congo ilisema kwenye Twitter kwamba “yote tabainika kuhusu chanzo cha janga hili na wale waliohusika watachukuliwa hatua.”  na kuongeza kuwa Rais Felix Tshisekedi aliamua mwezi uliopita juu ya “kuhamishwa kwa haraka kwa soko hilo kwa kuzingatia hatari iliyoko na eneo lake la sasa.”

Kampuni ya kitaifa ya kuzalisha umeme, SNEL, ilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba “radi ilikata nyaya za umeme.”

Afisa wa kampuni inayomilikiwa na serikali aliiambia AFP kwamba “sheria inakataza kujenga au kujenga chini ya nyaya za umeme, lakini wizara ya ardhi ilikuwa imetoa vibali vya kujenga katika maeneo haya kinyume cha sheria.”

Video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha maiti wakiwa waameanguka kwenye maduka ya soko huku miguu yao ikiwa imetumbukia kwenye maji yenye matope.

Christelle Zindo, mmoja wa wafanyabiashara hao alisema: “Kila wakati mvua inaponyesha, maji husalia hapa sokoni kwa sababu mtaro umeziba, na wafanyabiashara wote wanalazimika kufanya kazi huku miguu yao ikiwa kwenye maji.”

Miundombinu ya umeme katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mara nyingi haitunzwi.

Mjini Kinshasa, jiji kuu lenye zaidi ya watu milioni 10, wilaya kadhaa hukabiliwa na mafuriko wakati wa mvua kutokana na mifumo duni ya mifereji ya maji iliyojengwa katika enzi za ukoloni.