Timu ya taifa ya mchezo wa soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imefuzu kwenye fainali ya kombe la dunia, kwa mara ya kwanza, baada ya miaka 52, baada ya kuifunga Jamaica bao 1-0, katika mechi muhimu ya kufuzu iliyochezwa kwenye uwanja wa Guadalajara nchini Mexico, Jumanne tarehe 31, 3 2026

Bao la ushindi lilifungwa katika muda wa ziada na Axel Tuanzebe, beki wa zamani wa Manchester United, katika mechi hiyo ngumu, iliyoishi kwa DRC kuandikisha historia nyingine ya kurejea tena kwenye michuano hiyo mikubwa na kuleta furaha kubwa kwa mashabiki na raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ushindi wa DRC unamaanisha kuwa, bara la Afrika litakuwa na wawakilishi 10 katika michuano hiyo inayoanza kutifua vumbi mwezi Juni hadi Jumai katika nchi za Marekani, Cananda na Mexico.
DRC ilifika hatua hii baada ya kuifunga Nigeria katika mchuano muhimu kati ya timu za Afrika na baadaye kufuzu katika fainali na kukutana na timu kutoka bara lingine, ili kutafuta nafasi hiyo ya kufuzu.
Timu hiyo sasa inajiunga na Ureno, Colombia na Uzbekistan katika kundi moja kuwania kombe hilo la dunia.
Kombe la dunia litaanza rasmi tarehe 11 Juni mwaka 2026 na litaandaliwa katika mataifa matatu, Canada, Mexico na Marekani