‘Echoes Of War’ Tamthilia Ya Wanafunzi Wa Butere Girls Inayoipa Serikali ya Kenya Tumbo Joto

Tamthilia ya ‘’Echoes of War’’ ya Shule ya Wasichana ya Butere, inazidi kuzua hisia mseto nchini Kenya hususan kuhusu uhuru na haki ya kusema na udhibiti wa serikali.

Tamthilia hiyo, iliyoandikwa na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, imezungumzia pakubwa madhila, mahangaiko na hali ngumu ya Maisha wanayopitia kizazi cha vijana alamarufu Gen Z. Pia inazungumizia utawala na haki za kijamii. Matukio haya yametoa taswira mbaya katika tasnia hiyo ya Michezo ya Kuigiza la Kitaifa inayofanyika jijini Nakuru.

Mzozo ulianza Alhamisi wakati wanafunzi wa shule hiyo walikosa vifaa muhimu kwa ajili ya tamasha hiyo, ikiwa ni pamoja na mfumo wa vipaza sauti, vifaa vya kuigiza, ukosefu watazamaji, walimu wao na msimulizi kwa mchezo wa kuigiza bwana Malala. Wanafunzi hao walifika katika ukumbi wa kuigiza na badala yake kuimba wimbo wa taifa na kisha kuondoka ukumbini kwa ghadhabu. Walitoka nje kwa huzuni na kuanza kuimba nyimbo za kukashifu serikali.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega na mwandishi wa “Echoes of War’ Cleophas Malala

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi dhidi ya wanafunzi hao waliokuwa wakifanya maandamano baada ya kuzuiwa kuonyesha onyesho lao la ‘Echoes of War’ ambalo limekuwa kivutio nchini, katika tamasha la sanaa la National Drama Festivals.

Tamthilia hii, inayozungumzia mustakabali wa taifa baada ya vita kwa uongozi wa vijana, imekuwa kivutio kikubwa, ikielezea hali ya kisiasa na kijamii kwa kutumia mitindo ya kisasa kama teknolojia na mitandao ya kijamii. Hata hivyo, imeshuhudia upinzani mkali kutoka kwa serikali, ikiwemo polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya wanafunzi na wanahabari waliokuwa wakifuatilia tamasha hilo.

Malala, ambaye alikamatwa kwa madai ya kuingia shuleni kwa ajili ya kuangalia mazoezi ya tamthilia hiyo, alikamatwa na polisi lakini aliachiwa baadaye bila mashtaka yoyote. Baada ya kuachiliwa, Malala alielezea jinsi wasichana wa Shule ya Butere walivyoonyesha ujasiri mkubwa kwa kususia onyesho hilo, akisema kwamba walistahili pongezi kwa hatua yao ya kishujaa.

Mashirika ya haki za binadamu kama Kamati ya Haki za Binadamu ya Kenya (KHRC) na Amnesty International pia yamekosoa vikali vitendo vya serikali, na kudai kuwa ni uvunjaji wa haki ya kisanii na uhuru wa kujieleza. Viongozi wa kisiasa kama Kalonzo Musyoka na Eugene Wamalwa wameungana na mashirika hayo, wakisema kuwa hatua za serikali ni za kiunyanyasaji na zinadhoofisha uhuru wa sanaa nchini Kenya.

Tamthilia ya Echoes of War imezua mjadala mkubwa kuhusu haki ya vijana katika kuchangia mazungumzo ya kisiasa, huku serikali ikikabiliana na upinzani kutoka kwa wataalamu wa sanaa na wananchi kwa jumla.