Emir wa Qatar awakutanisha marais Paul Kagame na Tshisekedi

Marais wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameelezea dhamira yao ya kusitisha mapigano mara moja na bila masharti baada ya kufanya mazungumzo ya kushtukiza nchini Qatar Jumanne. Mkutano huo, uliofadhiliwa na Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, ulifanyika saa chache baada ya mazungumzo ya amani nchini Angola kuvunjika.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalithibitishwa katika taarifa ya pamoja kutoka Rwanda, DRC, na Qatar, yakisisitiza umuhimu wa kuendeleza mazungumzo kwa ajili ya amani ya kudumu. Hata hivyo, haijulikani ikiwa kundi la waasi la M23 litaheshimu kusitisha mapigano, kwani kwa sasa linadhibiti sehemu kubwa ya mashariki mwa DRC, ikiwemo miji yake miwili mikubwa.

Mapema Jumanne, jaribio la kuwezesha mazungumzo ya amani kati ya serikali ya DRC na M23 nchini Angola lilishindikana baada ya kundi hilo la waasi kujiondoa dakika za mwisho. M23 ilituhumu “taasisi fulani za kimataifa” kwa kuvuruga mchakato wa amani, hasa ikirejelea vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya baadhi ya viongozi wake muhimu.

Umoja wa Ulaya hivi karibuni uliwawekea vikwazo makamanda watatu wa jeshi la Rwanda, mkuu wa wakala wa madini wa Rwanda, na viongozi waandamizi wa M23, akiwemo kiongozi wake Bertrand Bisimwa, kwa kuhusika katika mgogoro wa mashariki mwa DRC. Kwa kujibu, M23 ilidai kuwa vikwazo hivyo vinadhoofisha juhudi za mazungumzo na kuituhumu serikali ya DRC kwa “kampeni ya uchochezi wa vita” inayozuia mazungumzo kufanyika.