Umoja wa Ulaya Jumanne uliahidi kuongeza euro milioni 600 kusaidia mataifa yaliyo hatarini kukabiliana na mzozo wa usalama wa chakula uliozidishwa na vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Fedha hizo ni pamoja na euro milioni 150 katika usaidizi wa kibinadamu kwa mataifa ya Afrika, Caribbean na Pacific na euro milioni 350 ili kuimarisha uzalishaji endelevu wa chakula kwa muda mrefu.
“Vita vya Urusi vinaleta madhara makubwa na yasiyo na maana, sio tu kwa wakazi wa Ukraine lakini pia wale walio hatarini zaidi kote duniani,” mkuu wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen alisema.
“Urusi bado inazuia mamilioni ya tani za nafaka zinazohitajika sana. Ili kuwasaidia washirika wetu tutakusanya euro milioni 600 za ziada ili kuepuka shida ya chakula na mshtuko wa kiuchumi.”
Mataifa ya Magharibi na Ukraine yanaishutumu Moscow kwa kujaribu kuwashinikiza wakubaliane kwa kuzuia usafirishaji muhimu wa nafaka kupitia Bahari ya black Sea ili kuongeza hofu ya njaa duniani.
Lakini EU imejitahidi kukabiliana na madai ya Kremlin, ambayo yanahusisha kupanda kwa bei na mapungufu katika Mashariki ya Kati na Afrika na vikwazo vya Umoja huo ilivyowekewa Urusi.
Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell siku ya Jumatatu alitaja kizuizi cha Urusi kama uhalifu wa kivita na kuonya kwamba Moscow itawajibika ikiwa itaendelea kusitisha mauzo ya nje.
EU inaunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kupatanisha makubaliano kati ya Ukraine, Urusi na Uturuki ili kupata nafaka, lakini hii imeshindwa kupiga hatua hadi sasa.
Brussels inajaribu kuongeza mauzo ya nje kutoka Ukraine kwa kutumia njia za reli, lakini hakuna uwezo wa kutosha wa kusafirisha kiasi cha mazao kilichpkwama.