Fahamu agenda ya mkutano wa kawaida wa 38 ya umoja wa Africa

Marais na viongozi mbalimbali barani Afrika wanawasili jijini Addis Ababa nchini Ethiopia kwa ajili ya Mkutano wao wa Umoja wa Afrika utakaofanyika Februari 15 na 16, 2025.

Wengi wa wajumbe wa mkutano huu, wanatokea nchi zenye wagombea wanaowania nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Kenya, Madagascar na Djibouti zinawania nafasi ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, huku nchi za Afrika Kaskazini zikiitolea macho nafasi ya makamu Mwenyekiti wa tume hiyo.

Wakuu wa nchi ndio watakaoshiriki kwenye uchaguzi huo, huku nchi 49 pekee ndizo zitakazoruhusiwa kupiga kura.

Nchi za Mali, Guinea, Burkina Faso, Gabon, Niger na Sudan hazitoshiriki mkutano huo wala kushiriki katika kumpigia kura mwenyekiti mpya wa AUC.

Hii ni kutokana na kuwa, mataifa hayo yako chini ya utawala wa kijeshi na bado hayajakabidhi madaraka kwa serikali za kiraia.

Wakati huo huo, ili Umoja wa Afrika upate mwenyekiti atakayechukua nafasi ya Moussa Faki kutoka Chad, ni lazima mshindi apate theluthi mbili ya kura 49, ili uchaguzi usirudiwe.

Hali kadhalika, viongozi hao wanakutana wakati mgogoro nchini DRC ukishika kasi na kuhatarisha hali ya usalama wa eneo la maziwa makuu.

Kuendelea kwa juhudi za upatanisho nchini Sudan ambako mapigano yameendelea tangu Aprili 2013 pia ni suala ambalo litaangaziwa wakati wa mkutano ndani ya kuta za Makao Makuu ya Umoja wa Afrika.

Suala la ukosefu wa usalama katika eneo la Sahel pia litajadiliwa wakati wa mkutano huo pamoja na njia zitakazotumika kuzishawishi nchi zilizo chini ya uongozi wa kijeshi kufanya uchaguzi na kukabidhi madaraka kwa serikali za kiraia.

People walk around at the AU Headquarters ahead of the 38th African Union (AU) Summit, where leaders will elect a new head of the AU Commission, in Addis Ababa on February 14, 2025. (Photo by Amanuel Sileshi / AFP)

Pia katika ajenda ya viongozi wa Afrika ni kutoa muelekeo wa namna gani mfuko wa amani wa Umoja wa Afrika, kuanzishwa kwa shirika la misaada barani na utekelezaji wa Eneo la Biashara Huru la Bara la Afrika.

Viongozi wa Afrika watatoa kipaumbele kwa mambo ya afya wakati bara la Afrika likikabiliana na magonjwa ya milipuko kama vile Ebola, Mpox na Marburg.