FAO: Bei ya vyakula duniani yaongezeka kutokana na vita vya Ukraine

Bei za vyakula duniani zilipanda sana kutoka mwezi Machi wakati uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ulipoathiri  masoko ya nafaka na mafuta ya kupikia, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa lilisema Ijumaa.

Kutatizika kwa mtiririko wa mauzo ya nje uliotokana na uvamizi wa Februari 24 na vikwazo vya kimataifa dhidi ya Urusi kumezua hofu ya mzozo wa njaa duniani, hasa katika Mashariki ya Kati na Afrika, ambako madhara makubwa tayari yameanza kujitokeza.

Urusi na Ukraine, ambazo kanda zake kubwa za nafaka ni miongoni mwa nchi zinazozalisha chakula kwa wingi duniani, zinachangia sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya dunia katika bidhaa kuu kadhaa, ikiwa ni pamoja na ngano, mafuta ya kupikia na mahindi.

“Bei za bidhaa za chakula duniani zilipanda kwa kiasi kikubwa mwezi Machi kufikia viwango vyake vya juu zaidi, wakati vita katika eneo la Black Sea vilisababisha bei kupanda katika masoko ya nafaka na mafuta ya kupikia,” FAO ilisema katika taarifa yake.

Fahirisi ya bei ya chakula ya FAO, ambayo tayari ilikuwa imeripoti ongezeko kubwa mwezi Februari, ilipanda kwa asilimia 12.6 mwezi uliopita, “ilipanda kwa kiasi kikubwa na kufikia kiwango kipya cha juu tangu kuanzishwa kwake mwaka 1990,” shirika la Umoja wa Mataifa lilisema.

Fahirisi, kipimo cha mabadiliko ya kila mwezi ya bei ya kimataifa ya kapu la bidhaa za chakula, ilifikia wastani wa pointi 159.3 mwezi Machi.

Kuongezeka huko kunajumuisha viwango vipya vya juu vya mafuta ya kupikia, nafaka na nyama, FAO ilisema, na kuongeza kuwa bei ya sukari na bidhaa za maziwa “pia ilipanda kwa kiasi kikubwa.”

 Hofu ya njaa

Urusi na Ukraine kwa pamoja zilichangia karibu asilimia 30 na asilimia 20 ya mauzo ya ngano na mahindi duniani mtawalia, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, FAO ilisema.

Vita vinaendelea kupamba moto huku msimu wa kupanda ukiwa umeanza nchini Ukraine.

Bei ya ngano ilipanda kwa karibu asilimia 20, huku tatizo hilo likizidishwa na wasiwasi juu ya hali ya mazao nchini Marekani, shirika hilo lilisema.

Fahirisi ya bei ya mafuta ya mboga ya FAO ilipanda kwa asilimia 23.2, ikisukumwa na nukuu za juu za mafuta ya alizeti, ambayo Ukraine ndiyo inayoongoza duniani kwa kuuza bidhaa nje.

Maduka ya jumla Uhispania yamepunguza uuzaji wa mafuta ya alizeti wakihofia uhaba kutokana na vita.

Amerika imemshutumu Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa kuanzisha “mgogoro huu wa chakula duniani”

Ufaransa imeonya kuwa vita hivyo vimeongeza hatari ya njaa duniani kote.

Mzozo huo pia umepelekea bei ya mafuta na gesi kuongezeka, na kusababisha mfumuko wa bei kupanda zaidi duniani kote na kuibua wasiwasi kwamba unaweza kudhoofisha ukuaji wa uchumi wa dunia.