Fulana aliyovaa mwanariadha Eliud Kipchoge katika mbio moja wapo alizoshiriki imenunuliwa katika mnada wa kimataifa kwa Ksh 242,472.
Kipchoge kwa ushirikiano na kampuni ya mnada ya Catawiki iliweka baadhi ya mavazi, viatu na saa zake Kipchoge kwenye mnada kwa lengo la kupata fedha za kufadhili elimu ya wanafunzi maskini kupitia wakfu wake wa Eliud Kipchoge.
Kati ya vitu vilivyowekwa mnadani ni fulana maalum iliyovutia bei ya juu kabisa na kununuliwa kwa Ksh.242,471
(€1,893).
Bidhaa nyingine iliyonunuliwa kwa kiasi kikubwa cha pesa ni kitambaa chenye nambari yake ya ushiriki wa mbio za BMW Berlin Marathon, kitambaa hicho kilinunuliwa kwa kiasi cha Ksh140,897 au (€ 1,100).
Viatu vya Eliud Kipchoge aina ya Nike- ZoomX Vaporfly Next% 2 vilinunuliwa kwa Ksh42393 au (€ 331). Viatu hivyo vilitiwa saini na ujumbe maalum kutoka kwake Kipchoge.
Chupa za maji mbili zilizotumiwa na Eliud Kipchoge wakati aliposhiriki mbio za masafa marefu zilinunuliwa kwa Ksh35,864 au (€ 280). Saa yake iliyokuwa na rangi za bendera ya Kenya ilikuwa pia mnadani na kununuliwa kwa Ksh48,673.
Kampuni ya mnada ya Catawiki, ilisema kuwa bidhaa zote zilizowekwa mnadani zinawakilisha nyakati muhimu katika miaka mingi ya riadha ya Eliud Kipchoge ikiwemo kitambaa maalum kilichokuwa na nambari yake ya ushiriki wa mbio za masafa marefu za Berlin 2018.
Eliud Kipchoge, mshindi mara mbili wa mbio za Olimpiki alizindua wakfu wake Septemba 9 akiamini wakfu huo utasaidia wanafunzi wengi katika jamii.
“Nina furaha sana kuzindua wakfu wangu wa Eliud Kipchoge,lengo langu likiwa kuwasaidia wanafunzi kupata elimu” Kipchoge alisema.