Fuvu la kichwa cha binadamu lagunduliwa baada ya shambulizi la fisi Kenya


Kundi la fisi limewaua watu wawili kwenye muda wa saa 24 katika kijiji kilichoko kilomita 50 tu mashariki mwa jiji la Nairobi, Kenya polisi wamesema Jumanne.
 
Fisi hao, takriban 20, walimjeruhi mwanamume mmoja siku ya Jumatatu katika kijiji cha Kamuthi karibu na mji wa Thika alipokuwa akirejea kutoka kazini kwake kwenye machimbo ya mawe, polisi wamesema.
 
Mwanamume mwingine aliyeandamana na mwathiriwa “aliponea chupuchupu,” polisi walisema kwenye Twitter.
 
Saa 24 baada ya shambulio la kwanza, fisi hao waliwashambulia watu wengine, wakazi walipata fuvu la kichwa cha binadamu katika moja ya mashamba kijijini humo.
 
Kulingana na ripoti ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), mkazi mmoja alipata fuvu la kichwa cha binadamu katika shamba lake lililopo Kandara Investment Scheme siku ya Jumatatu na kuripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Makongeni.
 
Baada ya hapo, maafisa kutoka polisi na Huduma ya Wanyamapori ya Kenya (KWS) walitembelea eneo la tukio ambapo walithibitisha kisa hicho.  

“Fuvu la kichwa, mifupa iliyotawanyika na nguo zilizochanika na kulowa damu zilipatikana,” Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ilisema, na kuongeza kuwa alama za nyayo za fisi zilionekana kwenye eneo hilo.

Ripoti za wanyamapori kuingia katika makazi ya binadamu nchini Kenya zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni huku wanyama hao wakikabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na kupanuka kwa miji hadi maeneo ya mbuga za wanyama pori.

Chui aliingia katika moja kusini mashariki mwa Kenya mnamo Desemba 17 baada ya kutoweka kutoka Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo kabla ya wahudumu wa KWS kumkamata.

Katika kisa kingine, simba alizua hofu mnamo Julai baada ya kutoka katika Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi na kuingia katika mtaa wenye watu wengi wa South C.

DCI imewasihi wakazi kuwa waangalifu huku uchunguzi kuhusu suala hilo ukiendelea ili kupata suluhu ya tatizo hilo.

“Tunawaomba wakazi katika maeneo yaliyotajwa kuendelea kuwa waangalifu na kujihadhari na wanyamapori hatari,” DCI alisema.