Gambia: Waziri wa zamani ameachiliwa huru baada ya madai ya mapinduzi

Gambia imemwachilia waziri wa zamani aliyezuiliwa wiki iliyopita huku serikali ikitangaza kuwa imezuia jaribio la mapinduzi, wakili wake alisema Ijumaa.

Mwanasiasa wa upinzani Momodou Sabally, waziri wa zamani wa masuala ya rais chini ya kiongozi wa zamani Yahya Jammeh, alionekana kwenye video akipendekeza rais wa sasa Adama Barrow angepinduliwa kabla ya uchaguzi ujao.

“Sabally ameachiliwa,” wakili wake Abdoulie Fatty alisema.

“Hajafanya kosa lolote, hivyo kumweka kizuizini ni kinyume cha sheria na ni ukiukwaji wa haki zake za kimsingi za binadamu.”

Serikali mnamo Desemba 21 ilisema ilikuwa imezuia jaribio la mapinduzi siku iliyotangulia, na mamlaka imewakamata wanajeshi saba.

Taifa hilo dogo la Afrika Magharibi mnamo Jumanne lilianzisha “jopo la uchunguzi” kuchunguza madai ya mapinduzi hayo.

Gambia ni demokrasia dhaifu, ambayo bado ina kovu na udikteta katili wa miaka 22 chini ya Jammeh.

Alishindwa katika uchaguzi wa urais mwezi Disemba 2016 na mgombea mpya wa kisiasa Barrow na kukimbilia Equatorial Guinea lakini bado ana nguvu nyumbani.

Barrow alichaguliwa tena Desemba 2021 kwa muhula wa pili wa miaka mitano katika koloni hilo la zamani la Uingereza, ambayo ni nchi ndogo zaidi katika bara la Afrika, inayozunguka mto unaoipa jina lake.

Ina ufuo mdogo wa Atlantiki lakini kwa njia nyingine imezungukwa na Senegal.