Hamas Yathibitisha Kifo cha Kiongozi Wao Yahya Sinwar

Kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas siku ya Ijumaa lilithibitisha kuwa kiongozi wao Yahya Sinwar aliuawa na jeshi la Israel huko Gaza, siku moja baada ya Israel kutangaza kifo chake.

“Tunaomboleza kiongozi mkuu, aliyeuawa shahidi, Yahya Sinwar, Abu Ibrahim,” afisa wa Hamas mwenye makao yake Qatar Khalil al-Hayya alisema katika taarifa ya video iliyorekodiwa iliyotangazwa na Al Jazeera.

Sinwar alikua anatafutwa sana na Israeli baada ya shambulio la Oktoba 7, 2023, ambalo lilikuwa baya zaidi katika historia ya Israeli.

Katika taarifa yake, Hayya alisema Hamas haitawaachilia mateka iliowakamata kutoka Israel wakati wa shambulio hilo hadi vita vya Gaza viishe.

Mateka “hawatarejea… isipokuwa vita dhidi ya watu wetu huko Gaza vikome,” afisa mkuu wa Hamas alisema, alipotoa wito kwa Israel kuondoka Gaza na kuwaachilia wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel.

Hayya alisema kundi hilo la wanamgambo litapata nguvu kutokana na mauaji ya Sinwar, ambayo alisema yamemweka miongoni mwa “viongozi na alama za vuguvugu waliomtangulia”.