Kundi la waasi la M23 katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limewaua raia 29 tangu katikati ya mwezi Juni katika maeneo yaliyokuwa chini ya udhibiti wao, Human Rights Watch ilisema Jumatatu.
Kundi la M23 ‘March 23 Movement’ lilipata umaarufu wakati liliteka kwa muda mji wa Goma mashariki mwa Congo mwaka 2012 kabla ya kufurushwa katika mashambulizi ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na Congo.
Baada ya kukaa kimya kwa miaka mingi, kundi hilo lilianza tena mapigano Novemba mwaka jana.
Waasi wamepiga hatua kubwa mashariki mwa Congo.
Mwezi uliopita, wapiganaji wa M23 waliuteka mji wa kimkakati wa Bunagana kwenye mpaka wa Congo na Uganda.
“Mashahidi waliiambia Human Rights Watch kwamba mnamo Juni 21, kufuatia mapigano kuzunguka kijiji cha Ruvumu, waasi wa M23 waliwaua takriban raia 17, wakiwemo vijana wawili, ambao waliwashutumu kwa kutoa taarifa kwa jeshi la Congo kuhusu nafasi zao na maficho yao,” HRW ilisema.
“Baadhi walipigwa risasi na kufa walipokuwa wakijaribu kukimbia,” mfuatiliaji wa haki alisema.
Vifo vingine vilitokea katika mashambulizi yaliyofuata katika kijiji kimoja na katika vitongoji vya Ruseke na Kabindi, na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 29, HRW ilisema.
“Tangu M23 wachukue udhibiti wa miji na vijiji kadhaa katika eneo la Kivu Kaskazini mwezi Juni, wamefanya aina kama hiyo ya unyanyasaji wa kutisha dhidi ya raia,” alisema mtafiti mkuu wa HRW Kongo Thomas Fessy.
DRC mara kwa mara imekuwa ikishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23, madai ambayo nchi hiyo imekuwa ikikanusha.
HRW ilisema kulikuwa na “wasiwasi ulioongezea” kwamba M23 “inapokea msaada kutoka kwa Rwanda kwa operesheni zake katika jimbo la Kivu Kaskazini.”
“Nchi wafadhili zinapaswa kusimamisha usaidizi wa kijeshi kwa serikali zinazopatikana kuwa zinaunga mkono M23 na vikundi vingine vinavyotumia silaha.” shirika hilo lenye makao yake makuu mjini New York lilisema.
HRW ilihimiza Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na wafadhili wa kimataifa wa DR Congo “kuunga mkono mkakati wazi wa kushughulikia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamua.”
Mkakati kama huo unapaswa kujumuisha ‘utaratibu wa ukaguzi wa huduma za usalama na kijasusi, utaratibu wa haki wa kimataifa, na mpango wa ulipaji wa kina, pamoja na mpango madhubuti wa uondoaji,” iliongeza.