Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya Oktoba 15, 2021 ni siku ambayo imeingia kwenye kalenda ya kumbukumbu ya maisha ya Lengai Ole Sabaya.Siku hii imeanzisha maisha mapya kwa Sabaya ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, baada ya kukutwa na hatia na kufungwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha akiwa yeye na wenzake.Hukumu hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na ghamu, imevuta hisia nyingi na kuibua mijadala mizito yenye maswali ya kutafakarisha mitandaoni na hata kwenye vijiwe vya wauza kahawa, lakini wengi wanaitazama hukumu ya Sabaya mbali zaidi wakihusisha na kesi iliyopo hivi sasa inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaotuhumiwa kwa kesi ya uhujumu uchumi yenye makosa ya ugaidi ndani yake.Kwenye mjadala huo wapo wanaoona sabaya kaonewa na wapo wanaona kuwa hukumu hiyo kwa Sabaya ni haki yake. Hata hivyo baadhi ya wakosoaji wanasema kwamba hukumu hii si ya kuifurahia kwani ni ya kujifunza na pia huenda ukawa ni mpango umepangwa huko mbele ukihusisha kesi ya Mbowe.