Idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko ndani na nje ya mji wa bandari wa Durban nchini Afrika Kusini imeongezeka hadi 306, serikali ilisema Jumatano, baada ya barabara na vilima kusombwa na maji huku nyumba zikiporomoka.
Mvua kubwa zaidi kuwahi kunyesha katika miaka 60 iliikumba manispaa ya Durban, inayojulikana kama eThekwini.
Dhoruba hiyo ndiyo mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Afrika Kusini.
“Kufikia jioni ya tarehe 13 Aprili, tumefahamishwa kwamba idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko katika jimbo la KZN (KwaZulu-Natal) imeongezeka hadi watu 306” Nonala Ndlovu, msemaji wa idara ya usimamizi wa maafa ya mkoa alisema.
Ofisi yake ilisema idadi ya vifo ni “mojawapo ya nyakati mbaya zaidi katika historia” ya KZN.
Mapema Jumatano Ndlovu alisema idadi ya waliokufa ni 259.
Rais Cyril Ramaphosa, ameelezea mafuriko kama “janga”
Takriban shule 248 zimeharibiwa na msako wa kuwatafuta watu waliopotea bado unaendelea, alisema Ramaphosa, na kuahidi kutoa msaada kwa walioathirika.
“Maafa haya ni sehemu ya mabadiliko ya hali ya hewa. Hatuwezi tena kuahirisha kile tunachohitaji kufanya … ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, uwezo wetu wa kukabiliana na maafa unahitaji kuwa katika ngazi ya juu,” alisema rais.
“Baadhi ya maeneo ya KZN yamepokea zaidi ya milimita 450 (inchi 18) za mvua katika saa 48 zilizopita,” alisema Tawana Dipuo, mtabiri wa huduma ya taifa ya hali ya hewa.
Hiyo ni sawa na karibu nusu ya mvua ya kila mwaka ya Durban ya mm 1,009.
Mvua iliendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo ya jiji Jumatano alasiri, na onyo la mafuriko lilitolewa kwa jimbo jirani la Eastern Cape.
Dhoruba hiyo ilipiga wakati Durban ilikuwa haijapata nafuu kutokana na machafuko mabaya Julai mwaka jana ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 350, katika machafuko mabaya zaidi nchini Afrika Kusini tangu kumalizika kwa ubaguzi wa rangi.
Jeshi la polisi la taifa lilipeleka askari 300 wa ziada katika mkoa huo, huku jeshi la anga likituma ndege kusaidia shughuli za uokoaji.
Zaidi ya nyumba 6,000 ziliharibiwa.
Mafuriko yaliua watu 140 mnamo 1995.