Idadi rasmi ya watu waliofariki kutokana na UVIKO 19 nchini India ilipita 500,000 siku ya Ijumaa, ingawa wataalam wengi wanaamini kuwa idadi halisi inaweza kuwa zaidi.
Taarifa ya kila siku kutoka kwa wizara ya afya ya shirikisho ilionyesha idadi ya walioaga ikifikia 500,055 na ongezeko la vifo 1,072 katika saa 24 zilizopita.
Jumla ya maambukizo imesalia katika milioni 41.9, kulingana na takwimu, India ikiwa nchi ya pili baada ya Amerika kwa idadi ya kubwa ya maambukizi ya UVIKO 19.
Idadi ya kesi imeongezeka katika wiki za hivi karibuni kutokana na maambukizi ya kirusi cha Omicron lakini viwango vya maabukizi mapya vimepungua katika siku za hivi karibuni.
Wataalam walisema wimbi la Omicron halitasababisha vifo vingi au watu kulazwa hospitalini, lakini majimbo kadhaa yaliweka marufuku ya kukabiliana na kuenea kwa kirusi hicho lakini sasa wameanza kuondoa marufuku hizo.
Mamlaka katika eneo la Delhi pamoja na mji mkuu mnamo Ijumaa walitangaza shule za upili, vyuo, mikahawa na kumbi za mazoezi zitaruhusiwa kufunguliwa kutoka wiki ijayo.
Baada ya kufungwa kwa karibu miaka miwili, kwanza kwa sababu ya UVIKO 19 na kisha tena kwa uchafuzi wa mazingira kufuatia kufunguliwa tena kwa muda mfupi, masomo kwa watoto wa miaka minne hadi 14 yataanza tena mnamo Februari 14, naibu waziri mkuu wa Delhi Manish Sisodia alisema kwenye ukurasa wake wa Twitter.
India ilikumbwa na ongezeko kubwa la visa vya UVIKO 19 mwaka jana kutokana na kirusi cha Delta ambacho kiliporomosha mfumo wake wa huduma za afya.
Wachambuzi wengi wanaamini kuwa watu 500,000 walifariki mwaka jana kutokana na ugonjwa huo.
Wimbi hilo lilishuhudia vifo vya takriban watu 200,000 huku hospitali zikikosa oksijeni na wagonjwa walihangaika kutafuta dawa.
Utafiti uliofanywa na kundi la utafiti la Amerika mwaka jana ulidokeza kuwa kati ya watu milioni 3.4 na milioni 4.7 walikuwa wamekufa.
Kwa miezi kadhaa sasa, majimbo kadhaa yamekuwa yakijumuisha idadi ya waliofariki na kuongeza vifo ambavyo vilikuwa havijaripotiwa huku Mahakama ya Juu ya India ikiamuru mamlaka za serikali kutoa fidia kwa familia zilizopoteza wapendwa wao kutokana na UVIKO 19.
Kerala, Bihar na jimbo alikotokea Waziri Mkuu Narendra Modi la Gujarat ni miongoni mwa majimbo yalioongeza maelfu ya vifo vya zamani kwenye orodha mpya.
Mwezi uliopita, serikali ya Modi iliyataka majimbo kuacha upimaji wa lazima wa watu ambao wamepima virusi, isipokuwa kama ni wadhaifu wa afya.
Lakini mara baada ya agizo hilo serikali iliambia majimbo kuongeza upimaji kadiri idadi ya maambukizi inavyopungua.
Kuongezeka kwa mauzo ya vifaa vya kujipima virusi vya UVIKO 19 nyumbani pia kumeongeza hofu ya visa vingi vya UVIKO 19 kutoripotiwa kote nchini.