Hatamu ya kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kama mwakilishi wa umoja wa Afrika katika maendeleo ya miundombinu ilifikia tamati katika njia tatanishi.
Taarifa za majukumu ya Odinga kutamatika katika Umoja wa Afrika yalitangazwa rasmi na mwenyekiti wa tume ya AU,Mousa Faki Mahamat ambaye alimshukuru odinga kwa kuwajibikia kazi yake.
Hata hivyo taarifa hii imekumbwa na wingu la maswali mengi yakiwemo iwapo Odinga alijiuzulu,alistaafu ama alifutwa kazi.
Katika barua ya kutangaza kuondoka kwa Odinga katika umoja wa Afrika iliandikwa Februari 19,Tarehe ambayo rais William Ruto aliondoka katika makao makuu ya AU Addis Ababa baada ya ziara ya siku mbili kuhudhuria makala ya 30 ya viongozi wa mataifa chama ya umoja wa Afrika.
Duru za kuaminika kutoka ofisi ya Umoja wa Afrika zinadai kuwa hatua hiyo Odinga “Kufutwa kazi” kulitokana na kile kinachotajwa kama msururu wa siasa ambazo waziri huyo mkuu wa zamani wa Kenya amekuwa akifanya nchini humo.
“Inafaa mkumbuke Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye alimsaidia kupata nafasi hiyo aliondoka mamlakani.Huku kulikuwa “kufutwa baridi” na ombi hili lilitolewa katika kikao cha faraghani ambacho kiliandaliwa baada ya mkutano wa AU Addisa Ababa Ethiopia,” alisema mfichuzi.
Inadaiwa kuwa Odinga pia alipoteza nafasi hii kuu barani Afrika kutokana na msimamo wake wa kisiasa ambapo amezidi kushikilia kuwa hamtambui Rais William Ruto na serikali ya Kenya Kwanza.
Mashambulizi ya mara kwa mara ya Odinga kwa serikali ya Rais Ruto akidai waliiba kura hata licha ya waangalizi wa kimataifa wakiwemo kutoka umoja wa Afrika (AU) kusimamia uchaguzi mkuu wa Agosti 9 2022 ambao waliutaja kuwa huru na wazi umemweka mashakani.
Tarehe 24 Februari 2023 Naibu wa rais nchini Kenya Rigathi Gachagua alionekana kupasua mbarika kwa kupigia mstari duru hizo kwa kuda kuwa alishindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na maandamano ya mara kwa mara na kuishambulia serikali.
“Maandamano yamefanya huyu mtu apoteze kazi kubwa katika Umoja wa Afrika.Wakati alikuwa anataftwa kufanya kazi yake hakupatikana ona amefukuzwa,” alisema Gachagua.
Odinga katika barua yake kwa umoja wa Afrika,aliwashukuru kwa kukubali ombi lake la kumruhusu kushughlikia majukumu mengine ya kibinafsi.
Odinga aliteuliwa katika wadhifa huo Oktoba 20, 2018 wakati wa utawala wa aliyekuwa rais wa nne wa jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta.
Kiongozi huyo alikuwa na afisi mbili, moja jijini Nairobi Kenya na nyingine jijini Addis Ababa Ethiopia ambapo makao makuu ya AU yapo.