Indonesia: Mamia ya watu wakimbia makazi yao baada ya volkano kulipuka


Mlima Merapi nchini Indonesia ulilipuka na kutoa moshi mwingi mwekundu na moto, na kugeuza anga katika eneo hilo kuwa nyekundu, huku lava iliyoyeyuka ikitirirka siku ya Alhamisi .

Mlipuko huo uliwalazimu zaidi ya watu 250 kukimbia makazi yao, mamlaka ilisema.

Volkano hiyo — ililipuka mara kadhaa katika usiku mmoja, ikitoa gesi, majivu ya volkeno na mawe ambayo yalitiririka zaidi ya kilomita tano, mkuu wa Shirika la Kitaifa la Kudhibiti na Kukabiliana na Majanga la Indonesia alisema.

“Kutokana na kutiririka kwa lava na majivu moto, watu 253 walihama makazi yao,” Abdul Muhari alisema katika taarifa yake.

Wakaazi wameambiwa waondoke kwenye eneo linalokaribiana na mlima huo kwa umbali wa kilomita saba ili kuepukana na lava na jivu la sumu ambalo bado linaendelea kutirirka kutoka mlima Merapi, Muhari aliongeza.

Mawingu moto na moshi kutoka kwa mlipuko huo ulitanda anga katika sehemu za Kisiwa cha Java chenye watu wengi, karibu na mji mkuu wa kitamaduni wa Indonesia Yogyakarta.

Mlima Merapi uko katika kiwango chake cha pili cha tahadhari tangu Novemba 2020 baada ya kuonyesha dalili mpya za kulipuka.

Mlipuko wake mkubwa wa mwisho ulifanyika 2010 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300 huku takriban wakaazi 280,000 kutoka maeneo ya karibu wakiyahama makazi yao.

Huo ulikuwa mlipuko wake mkubwa zaidi tangu 1930, ambao uliua karibu watu 1,300.
Mlipuko wa 1994 ulisababisha vifo vya watu wapatao 60.

Taifa la visiwa vya Kusini-mashariki mwa Asia lina karibu volkano 130 zinazoweza kulipuka wakati wowote ule.