Mkuu wa polisi nchini Kenya alitangaza Jumapili kupiga marufuku maandamano mapya ya upinzani yaliyoitishwa Jumatatu, baada ya maandamano ya wiki iliyopita kubadilika na kuwa ghasia.
“Hatutaruhusu maandamano yenye vurugu,” Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome aliwaambia wanahabari. “Maandamano wanayopanga kesho (Jumatatu) ni kinyume cha sheria na hayataruhusiwa.”
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amewataka watu kujitokeza barabarani siku ya Jumatatu na Alhamisi kwa maandamano zaidi kupinga kupanda kwa gharama ya maisha nchini Kenya.
Maandamano ya Jumatatu iliyopita, ambayo pia hayakuidhinishwa na polisi, yalizua vurugu, huku polisi wa kutuliza ghasia wakiwarushia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha watu waliokuwa wakirusha mawe na kuchoma matairi.
Mwanafunzi wa chuo kikuu aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi huku maafisa 31 wakijeruhiwa katika mapigano jijini Nairobi na ngome za upinzani magharibi mwa Kenya.
Zaidi ya watu 200 walikamatwa Jumatatu iliyopita, wakiwemo wanasiasa kadhaa wakuu wa upinzani, huku msafara wa Odinga mwenyewe ukipigwa na mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.
“Nyote mliona kilichotokea wiki iliyopita na hatutaruhusu hilo kutokea tena ambapo wahuni wanakuja mjini kupora na kuharibu mali na biashara za watu,” Koome alisema.
Ilikuwa ni ghasia za kwanza kuu za kisiasa tangu Rais William Ruto aingie madarakani miezi sita iliyopita baada ya kumshinda Odinga katika uchaguzi ambao mpinzani wake alidai kuwa “aliibiwa”.
Wakenya wengi wanatatizika huku wakikabiliana na bei ya juu ya bidhaa za kimsingi pamoja na kuporomoka kwa sarafu ya nchi hiyo na ukame ambao umewaacha mamilioni ya watu wakiwa na njaa.
Ruto, ambaye anaondoka nchini Jumapili kwa safari ya kuelekea Ulaya, amemtaka kiongozi wa upinzani kusitisha hatua ya maandamano.
“Ninamwambia Raila Odinga kwamba ikiwa ana shida nami, anapaswa kunikabili na aache kutia hofu nchi,” alisema Alhamisi.