Iran imewanyonga wanaume wawili mashoga baada ya kupatikana na tuhuma za kulawiti baada ya kukaa miaka sita kwenye hukumu ya kifo shirika la kutetea haki za binadamu liliripoti.
Mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria nchini Iran, hii ikiwa mojawapo ya maeneo yenye ukandamizaji mkubwa wa watu wa makundi ya LGBTQ.
Kulingana na ripoti ya Jumapili ya Human Rights Activists News Agency, watu hao wawili walitambuliwa kama Mehrdad Karimpour na Farid Mohammadi.
Walihukumiwa kifo kwa “kulazimishwa kufanya ngono kati ya wanaume wawili” na kunyongwa katika gereza moja katika mji wa kaskazini-magharibi wa Maragheh, takriban kilomita 500 kutoka mji mkuu, Tehran.
Julai iliyopita, wanaume wengine wawili walinyongwa kwa mashtaka sawa na hayo huko Maragheh, kundi hilo lilisema. Kundi hilo limeongeza kuwa mwaka jana, Iran iliwanyonga watu 299, wakiwemo wanne waliopatikana na hatia ya uhalifu waliotenda wakiwa watoto. Pia mnamo 2021, Iran ilihukumu watu 85 kifo.
Oktoba mwaka jana, mpelelezi huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Iran, Javaid Rehman aliiambia kamati ya haki za binadamu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba Iran inaendelea kutekeleza hukumu ya kifo “kwa kasi ya kutisha.”
Chini ya sheria za Iran, kulawiti, ubakaji, uzinzi, wizi wa kutumia silaha na mauaji ni miongoni mwa uhalifu unaoweza kusababisha hukumu ya kifo.