Israel itachangia chanjo milioni 1 za kukabiliana na UVIKO 19 kwa mpango wa COVAX.


Serikali ya Israel siku ya Jumatano ilisema itachangia chanjo milioni 1 za kukabiliana na virusi vya corona kwa mpango unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wa COVAX.

Wizara ya Mambo ya Nje ilisema chanjo za AstraZeneca zitasafirishwa katika wiki zijazo, uamuzi ambao ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wa Israeli na nchi za Kiafrika.

“Nimefurahi kuwa Israeli inaweza kuchangia na kuwa mshirika katika kutokomeza janga hili ulimwenguni,” Waziri wa Mambo ya nje Yair Lapid alisema.

Tangazo hilo lilisema kuwa chanjo hizo zitafikia karibu robo ya nchi za Afrika, ingawa haikutoa orodha ya nchi hizo. Israel ina uhusiano wa karibu na mataifa kadhaa ya Afrika, zikiwemo Kenya, Uganda na Rwanda.

Israel pia ilianzisha uhusiano na Sudan mwaka jana kama sehemu ya mfululizo wa mapatano yaliyopitishwa na Amerika.

COVAX ni mpango wa kimataifa ambao unalenga kutoa chanjo ya coronavirus kwa mataifa maskini. Nchi tajiri zaidi zimepata chanjo zaidi duniani, na kusababisha ukosefu mkubwa  katika upatikanaji wa chanjo hizo kwa mataifa mengine.

Israel ilikuwa moja ya nchi za kwanza duniani kutoa chanjo kwa watu wake. Mapema mwaka huu, ilikosolewa kwa kutogawa chanjo hizo kwa Wapalestina.

Tangu wakati huo, Israel imechanja maelfu ya Wapalestina wanaofanya kazi nchini Israel na kwenye makazi yake, na Wapalestina wamenunua chanjo kutoka COVAX na kutoka vyanzo vingine.