Mahakama ya kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku ya Ijumaa iliwafunga wasanii wawili wakufoka kwa miaka 10 na miwili kwa kukosoa jeshi na rais katika nyimbo zao.
Waimbaji wote wawili wamelaani kushindwa kwa serikali kukomesha umwagaji damu katika eneo la mashariki mwa nchi lililokumbwa na mzozo.
Idengo mwenye umri wa miaka 32, ambaye jina lake halisi ni Katembo Delphin, alihukumiwa kifungo cha miaka 10 kwa kosa la kulitusi jeshi.
Hukumu hiyo imetolewa na mahakama ya kijeshi katika gereza kuu la Goma, mji mkuu wa mkoa wa mashariki wa Kivu Kaskazini. Idengo alikamatwa mwezi Oktoba.
Muyisa Nzanzu Makasi mwenye umri wa miaka 33, alipewa miaka miwili kwa kumdharau mkuu wa nchi.
Jamaa wa watu hao wawili waliangua kilio, na upande wa utetezi ukatangaza mara moja kwamba watakata rufaa.
Kesi hiyo ilipofunguliwa mwishoni mwa mwezi Novemba, Idengo alisema anasimamia kila alichokisema kwenye nyimbo zake.
Nyumbani katika mji wa mashariki wa Beni, “watu wameuawa kila siku tangu 2014 — hakuna kilichobadilika,” alisema.
Makasi alikumbuka kwamba wakati wa kampeni za uchaguzi za Rais Felix Tshisekedi, “aliahidi kukomesha mauaji hayo,” “Lakini hakuna kilichobadilika,” alisema.
Mashariki mwa DRC inapambana na makundi mengi yenye silaha, mengi ya makundi hayo yakiwa ya kikanda ambayo yalizuka robo karne iliyopita.
Kivu Kaskazini haswa imekumbwa na mauaji yaliyotekelezwa na kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF) — kihistoria kundi la Kiislamu la Uganda ambalo Amerika mwaka huu ililihusisha rasmi na kundi linalojiita Islamic State.