Jamhuri yakimbilia Mahakama ya Rufani Baada ya Mahakama Kuu Kukataa Ushahidi  wa Nyongeza

Upande wa Jamhuri umepeleka maombi ya mapitio katika Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi mdogo wa Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, uliokataa kupokelewa kwa ushahidi wa nyongeza wa shahidi mpelelezi, ACP Amini Mahamba katika kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu.

Jamhuri yakimbilia Mahakama ya Rufani Baada ya Mahakama Kuu Kukataa Ushahidi  wa Nyongeza

Akiwasilisha taarifa hiyo leo mahakamani muda mfupi baada ya uamuzi  kutolea juu ya pingamizi la nyongeza ya ushahidi, pingamizi ambalo limetolewa na Lissu, Wakili Mkuu wa Serikali Renatus Mkude alisema baada ya mahakama kutoa uamuzi huo na kuutafakari Mkurugenzi wa Mashtaka alimepeleka maombi ya kupitiwa kwa uamuzi huo kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha sheria ya Mahakama ya Rufani Tanzania.

“Serikali tuliomba lisaa limoja kwa ajili ya tafakuri ya yale maamuzi tukidhani tutamaliza mapema,” alisema Mkude na kuongeza.

“Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP) kwa niaba ya Jamhuri amewasilisha taarifa ya mapitio kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Sura ya 141 (Marejeo ya 2023) pamoja na Kanuni ya 65(1) ya Kanuni za Rufani”Mkude aliiambia mahakama kuwa maombi hayo yanaungwa mkono na kiapo cha Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi, na tayari yamesainiwa na kuwasilishwa kwa njia ya kielektroniki Mahakama ya Rufani, yakasajiliwa kwa namba 7203216/2026.

“Kwa kuwa shauri hili limeshapokelewa Mahakama ya Rufani na kupewa namba, ni rai yetu kwamba shauri hili lisimame ili kupisha uamuzi wa mahakama hiyo,” alieleza.

Akijibu hoja hiyo, mshtakiwa Tundu Lissu anayejitetea mwenyewe, aliomba apewe nakala ya “Notice of Motion” akieleza kuwa yupo gerezani hivyo uwezekano wankuipata kwa njia ya mtandao ni ngumu.

Aidha, alirejea Kifungu cha 8(2)(d) cha Sheria ya Mahakama ya Rufani akidai hakiruhusu rufaa au mapitio ya maamuzi yasiyomaliza shauri la msingi.

“Ninafahamu kwamba kwa mujibu wa kifungu hicho, hakiruhusu rufaa wala mapitio ya maamuzi ambayo hayamalizi shauri la msingi,” alisema.

Hata hivyo, aliongeza kuwa hakuwa akiiomba mahakama hiyo kutoa uamuzi kuhusu hoja hiyo kwa kuwa suala hilo sasa liko Mahakama ya Rufani na majaji wameshafungwa mikono.

“Waheshimiwa majaji siwaombi mtoe uamuzi wowote kwenye hili kwa sababu mikono yenu imefungwa, shauri inabidi liende kule,” alisema.

Lissu pia alidai kuwa lengo la kuwasilisha mapitio hayo ni kurefusha shauri ili aendelee kukaa gerezani huku akisisitiza kuwa yeye hana hatia.

“Ninafahamu lengo la kupeleka maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani ni kurefusha shauri ili niendelee kukaa gerezani. Kwa vile wananipeleka huko, nitawafuata huko huko,” alisema.

Katika hoja ya ziada, alilalamikia kutoruhusiwa kuzungumza faragha na mawakili wake wanapomtembelea gerezani jambo ambalo amekua akilizunguza zaidi ya mara moja Mahakamani.

Hatua ya Jamhuri kupeleka maombi ya kutaka mapitio ya uamuzi wa pingamizi la Lissu uliokataa nyongeza ya ushahidi kwa shahidi wao  imekuja baada ya Mahakama Kuu kukubali pingamizi la Lissu la kupinga taarifa ya kuongeza ushahidi (notice) iliyowasilishwa Februari 18, 2026 chini ya Kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20 (Marejeo ya 2023).

Upande wa mashtaka ulikuwa umekusudia kuwasilisha ushahidi wa nyongeza wa ACP Mahamba, ikiwemo maelezo aliyoyatoa wakati wa uchunguzi kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya jopo la majaji, Jaji Dastun Ndunguru alisema mahakama imepitia hoja za pande zote, vifungu vya sheria husika na kumbukumbu za mwenendo wa kesi.

“Kifungu cha 308 kinafungua mlango wa kumuita shahidi na maelezo yake, lakini hakifungui mlango wa kuleta shahidi mpya au ushahidi mpya ambao haukuwepo katika hatua za awali,” alisema Jaji Ndunguru.

Mahakama ilibaini kuwa notice iliyowasilishwa na Jamhuri ilikuwa ya maelezo ya nyongeza yasiyoangukia katika masharti ya kifungu hicho, hivyo haikuwa na msingi wa kupokelewa katika hatua ya sasa ya shauri.

Kutokana na uamuzi huo, mahakama ilikubaliana na pingamizi la mshtakiwa na kukataa maombi ya Jamhuri ya kuingiza ushahidi huo wa nyongeza.

KESI YASIMAMISHWA KUSUBIRI UAMUZI WA MAHAKAMA YA RUFANI Baada ya kusikiliza hoja za pande zote kuhusu hatua ya mapitio, mahakama ilisema kuwa kutokana na shauri hilo kupokelewa Mahakama ya Rufani, kesi hiyo itasimama hadi pale shauri lililoko Mahakama ya Rufani litakapomalizika.

Mpaka sasa katika kesi ya msingi ya Uhaini inayomkabili Lissu, upande wa Jamhuri umeleta mashahidi 15 kati ya mashahidi 30 waliokuwa nao.