Mwanasheria wa Serikali, Nassoro Katuga, ameanza kumuuliza maswali ya dodoso Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, katika hatua ya kuhojiwa kuhusu ushahidi alioutoa mbele ya Mahakama katika kesi inayomkabili.

Katika maswali hayo, Katuga amejikita katika elimu na taaluma ya Lissu, nafasi yake kisiasa, uelewa wake wa sheria, hotuba aliyotoa Aprili 3, pamoja na kauli mbalimbali alizotoa kuhusu uchaguzi na maandamano.
Akianza, Katuga amempongeza Lissu kwa ushahidi mrefu alioutoa, huku akimweleza Mahakama kuwa hatua hiyo ya kumuuliza maswali ni sehemu ya utaratibu wa kisheria.
Lissu amekubaliana na kauli hiyo.
Katuga pia amemuuliza Lissu kuhusu taaluma yake ya sheria, ambapo Lissu amekiri kuwa ni mwanasheria na ana ujuzi wa masuala ya sheria.
Katika maswali ya awali, Katuga amemuuliza Lissu kuhusu uhuru wa Tanzania, ambapo Lissu amesema Tanzania ilipata uhuru Desemba 9 na kwamba ni nchi huru.
Alipoulizwa Mahakama ni chombo cha mwisho chenye mamlaka ya kutoa maamuzi, Lissu amesema ni Mahakama ya Tanzania.
Katuga pia amemuuliza Lissu kuhusu hoja aliyoitoa katika ushahidi wake kwamba akiwa Mwenyekiti wa CHADEMA ana kinga fulani, jambo ambalo Lissu amekanusha na kusema hajawahi kuiambia Mahakama kwamba nafasi yake kama Mwenyekiti wa chama inampa kinga hiyo.
Katuga amerejea sehemu ya ushahidi wa Lissu kuhusu tuzo mbalimbali alizowahi kupata na kumuuliza kama tuzo hizo ziliwasilishwa Mahakamani kama ushahidi.
Lissu amejibu kuwa hakuwasilisha tuzo hizo.
Katika eneo hilo, Katuga amemuuliza Lissu kwa nini hakuwasilisha nyaraka mbalimbali ambazo angeweza kuzitumia katika utetezi wake.
Lissu amesisitiza kuwa hana wajibu wa kuthibitisha kesi hiyo, akirejea misingi ya sheria ya ushahidi.
Katuga amemuuliza Lissu kifungu maalumu cha sheria kinachompa wajibu huo, lakini Lissu amejibu kwa kurejea misingi ya sheria za ushahidi.
Katika hatua nyingine, Katuga amesoma baadhi ya maneno ambayo Lissu aliwahi kuyasema katika hotuba yake na kumuuliza kama anakubaliana kuwa maneno hayo ni yake.
Lissu amekanusha kuwa alisema baadhi ya maneno hayo.
Hata hivyo, alipoulizwa kama anayakataa maneno hayo, Lissu amesema hayakatai kwa sababu, kwa mtazamo wake, hayakuwa kosa wala hayakuwa na tatizo.
Katuga pia amemuuliza Lissu kuhusu historia ya ukoloni na namna ambavyo baadhi ya watawala wa kikoloni walivyotumia viongozi wa maeneo husika katika kutawala.
Katuga amerejea pia katika historia ya Lissu kama mtetezi wa masuala ya rasilimali, akimuuliza kuhusu msimamo wake wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano kuhusu usafirishaji wa makinikia.
Lissu amekanusha kwamba aliwahi kusema makinikia yatoke nchini.
Katuga amemuuliza pia kama wakati fulani alipokuwa akishtakiwa alikuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), jambo ambalo Lissu amelikataa.
Lissu amesema amekuwa akitetea rasilimali za nchi na amesisitiza kuwa alikuwa mwaminifu katika mapambano hayo.
Katika sehemu nyingine ya dodoso, Katuga amemuuliza Lissu kuhusu njia za kikatiba na kisheria za kupinga jambo, ikiwemo kupitia maandamano na vyombo vya habari.
Lissu amerejea Ibara ya 20(1) ya Katiba akieleza kuwa inaweka msingi wa uhuru huo.
Katuga pia amemuuliza Lissu kama anamfahamu wakili Julius Ishengoma, ambapo Lissu amekiri kumfahamu na kumtaja kama mwanasheria aliyewahi kufungua shauri kuhusu kiwango cha fedha.
Aidha, Lissu amerejea historia ya kesi ya mgombea binafsi akimtaja Christopher Mtikila, ambaye alisema alishinda katika Mahakama Kuu kabla ya uamuzi huo kubadilishwa na Mahakama ya Rufani, na baadaye akaenda katika Mahakama ya Afrika ambako alishinda.
Katuga pia amemuuliza kuhusu Rugemeleza Nshala, ambapo Lissu amesisitiza kuwa si shahidi wake katika kesi hiyo.
Katuga amerejea katika kifungu cha 39 cha Kanuni ya Adhabu, akimuuliza Lissu kuhusu maana ya “manifestation” na njia zake.
Lissu amesema zipo njia mbili, akitaja “publication” kama mojawapo.
Wakili Katuga amemuuliza kama maneno hayo yanapotumika katika mazingira ya kesi hiyo yanaweza kuwa na maana moja au tofauti.
Lissu amesema yanaweza kuambatana au yasifanane, kutegemea mazingira.
Katuga pia amemkabili Lissu kuhusu kauli zake kuhusu Serikali na kumuuliza kama, kutokana na ushahidi alioutoa kuhusu matukio yaliyompata, itakuwa sahihi kusema kwamba ana chuki dhidi ya Serikali.
Lissu amejibu:
“Nina chuki dhidi ya uonevu wa Serikali.”
Katuga amemuuliza Lissu kama, kwa kuwa yeye ni mwanasiasa, anakubaliana kwamba mojawapo ya malengo ya chama cha siasa ni kushika dola.
Lissu amesema hilo ni moja ya malengo ya chama cha siasa.
Katuga kisha amemuuliza kuhusu mihimili mitatu ya dola.
Lissu ametaja Serikali, Mahakama na Bunge.
Alipoulizwa kazi ya Bunge, amesema mojawapo ni kutunga sheria, huku akieleza kuwa jukumu la Mahakama ni kutafsiri sheria.
Katuga pia amerejea tena kifungu cha 39 cha Kanuni ya Adhabu na kumuuliza Lissu kama, kwa tafsiri yake ya kisheria, ili kuthibitisha kosa hilo ni lazima Serikali iwe imetishika.
Lissu amejibu kwa neno moja:
“Hakuna.”
Katika sehemu nyingine ya maswali, Katuga amemuuliza Lissu kama aliwataja Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCP) na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kuwa mashahidi wake.
Lissu aliwataja
Hata hivyo, alipoulizwa kama hao ni mashahidi wema, Lissu amekataa kutumia neno hilo na kusema aliwaita kwa sababu wanafahamu ukweli kuhusu kesi hiyo.
Katuga amemuuliza pia Lissu kuhusu dhumuni la hoja za awali katika kesi.
Lissu amesema ni kuchambua masuala yanayobishaniwa na yale ambayo hayabishaniwi.
Sehemu kubwa ya maswali ya Katuga imejikita katika hotuba ambayo Lissu aliitoa Aprili 3, ambapo amethibitisha kuwa alitoa hotuba mbele ya watia nia wa CHADEMA na waandishi wa habari.
Katuga amemuuliza kama katika ushahidi wake Lissu aliwahi kuwaambia waandishi wa habari warekodi hotuba hiyo kwa ajili ya kuipeleka kwa jamii.
Lissu amesema hakuwambia wafanye hivyo.
Hata hivyo, alipoulizwa kama kwa mantiki hiyo alitaka hotuba yake isambae kwa wananchi, Lissu amekubali.
Katuga amemuuliza pia kama wakati akitoa hotuba hiyo aliweka mipaka kwamba watu fulani wasisikie na wengine wasisikie.
Lissu amesema hakufanya hivyo.
Amesema pia watu aliokuwa akiwahutubia walikuwepo wakati akitoa hotuba hiyo.
Katuga amerejea ushahidi wa shahidi mwingine, P17, aliyesema watu walikuwa wakirekodi hotuba hiyo moja kwa moja, jambo ambalo Lissu amelikubali.
Katuga amemuuliza Lissu kama mtu anayesikiliza hotuba ana haki kuitafsiri kwa namna alivyoielewa.
Pia amekubali kwamba mtu huyo anaweza kuchukua hatua kulingana na namna alivyoielewa hotuba hiyo.
Katuga amemuuliza kama kauli za “tutazuia na kuvuruga uchaguzi” zinaweza kumaanisha kwamba kila mtu ana haki ya kuvuruga uchaguzi kwa namna alivyoielewa.
Lissu amekubali.
Katuga pia amerejea ushahidi wa PW3 aliyesema kulikuwa na mipango ya kupiga watu mawe na kuwazuia kwenda kupiga kura, ambapo Lissu amesema anakumbuka ushahidi huo.
Alipoulizwa kama uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa sheria, Lissu amesema:
“Upo kwa mujibu wa sheria.”
Katuga amemuuliza kama kuwazuia watu kwenda kupiga kura ni uvunjifu wa amani.
Lissu amekubali kwamba ni uvunjifu wa amani na uvunjifu wa sheria.
Katika swali lililofuata, Katuga amemuuliza Lissu kama, katika hotuba hiyo, alikuwa akihamasisha maandamano ya kidemokrasia.
Dodoso la Jamhuri linaendelea huku Lissu akiendelea kujibu maswali yanayolenga kuunganisha kauli zake, hotuba ya Aprili 3 na tafsiri ya kisheria ya vifungu vinavyohusiana na mashtaka yanayomkabili.
Kesi imeahirishwa mpaka kesho Agosti 27, 2026 saa tatu asubuhi.