Je, mwanamume huyu kutoka Eritrea ndio mzee zaidi kuwahi kuishi?

Natabay Tinsiew

Mwanamuwe kutoka Eritrea ameaga dunia akiwa na umri wa mika 127, familia yake imesema, ikitumai kuwa Natabay Tinsiew ataorodheshwa katika kitabu cha Guinness World Records kama mtu mwenye umri mkubwa zaidi duniani.

Mjukuu wake Zere Natabay, amesema siri ya babu yake kuishi kwa miaka mingi ilikuwa ni kuwa mvumilivu,mkarimu na kuwa mtu mwenye furaha.

Bwana Tinsiew aliaga dunia siku ya Jumatatu 27 Septemba katika kijiiji cha Azefa, kijiji chenye takriban watu 300.

Mjukuu wake Zere Natabay, anasema anarekodi za kanisa, ikiwemo cheti chake cha kuzaliwa kinachoonesha kuwa alizaliwa mwaka wa 1894, pamoja na mwaka aliobatizwa ikithibitisha aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 127.

Lakini familia yake inaamini alizaliwa mwaka wa 1884, na kubatizwa miaka kumi baadae wakati kasisi alipotembelea kijiji chao.

Kasisi Mentay, kasisi wa kanisa katoliki aliyehudunu katika kijiji hicho kwa miaka saba, amethibitisha kuwa bwana Natabay alizaliwa mwaka wa 1894, na kuwa alihudhuria sherehe za kuzaliwa za bwana Natabay aliposheherekea miaka 120 mwaka wa 2014.

Mjukuu wake, bwana Zere amesema amewasiliana na Guinness World Records ili kudhibitisha nyaraka rasmi za kuzaliwa kwake na anasubiri kusikia kutoka kwao. Guiness World Records imemuorodhesha mwanamke wa Ufaransa Jeanne Calment,aliyeaga dunia mwaka kwa 1997 akiwa na umri wa miaka 122 kama mtu mzee zaidi kuwahi kuishi.

Bwana Natabay alioa mwaka wa 1934 na mkewe akaaga dunia mwaka wa 2019 akiwa na umri wa miaka 99.

Bwana Zere amesema babu yake atakumbukwa kama mtu mwenye roho nzuri, mkarimu na mwenye bidi maishani.