Search
Close this search box.
Africa

Kwa kawaida katika mataifa mengi duniani, ndoa zilizozoeleka ni ndoa kati ya mume mmoja ma mke mmoja. Katika tamaduni ya mataifa mengi barani Afrika na katika mataifa ya kiislamu ndoa kati ya mume mmoja na wake wengi pia ni jambo la kawaida.

Lakini je, unafahamu kunako tamaduni ambazo ndoa kati ya mke mmoja na wanaume wengi ni jambo la kawaida?

Mapema mwaka huu, serikali ya Afrika Kusini ilipendekeza kuwepo kwa ndoa kati ya mwanamke mmoja na wanaume wengi. Pendekezo hilo lilipata pingamizi kubwa kutoka kwa wanaume nchini humo.

Ikumbukwe kuwa Afrika Kusini ni nchi ambayo inakubali ndoa kati ya mume mmoja na wake wengi, mfano rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma ana wake wanne. Ndoa kati ya watu wa jinsia moja pia inaruhusiwa katika sheria za nchi hiyo, mfano mwanariadha maarufu Caster Semenya alifunga pingu za maisha na mkewe Violet Raseboya mwaka wa 2015.

Caster Semenya na mke wake Violet Raseboya

Kwa hiyo ilikuwa jambo la kushangaza sana wakati pendekezo la kuruhusu ndoa kati ya mwanamke mmoja na wanamume wengi lilipopata pingamizi kubwa hususan kutoka kwa wanaume.

Mfanyabiashara na mtangazaji maarufu Musa Mseleku, ambaye ana wake wanne alikuwa mmoja wa wale waliopinga vikali pendekezo la wanawake kuolewa na wanamume wengi.

“Pendekezo hilo litahatarisha tamaduni za kiafrika,” alisema Mseleku.

Wanaharakati wa haki za kibinadamu walisema “iwapo tutadai kutambulika kwa ndoa tofauti itabidi ndoa kati ya mke mmoja na wanaume wengi pia ikubalike.”

Mataifa mengine Afrika ambako ndoa kati ya mke mmoja na wanaume wengi inakubaliwa ni katika kabila la Irigwe kutoka Nigeria Kaskazini.Wanawake katika jamii hii huishi kwa muda fulani kwa mume mmoja na kisha mume mwingine, na huwazalia waume wake wote.

Katika jamii ya waTibet kutoka China, inaaminika kuwa mwanamke anaweza kupata ujauzito kwa wakati mmoja kutoka kwa mbegu tofauti za wanaume, hivyo basi ndoa kati ya mwanamke mmoja na wanaume wengi ni jambo la kawaida. WaTibet maskini pia hufurahia tamaduni ya wanaume wengi kumuoa mwanamke mmoja kwa kuwa huepusha ugomvi wakati wa urithi kwani watoto wote wanakuwa wa jamii nzima wasijulikane baba yao ni nani haswa.

Familia ya mke mmoja na waume watatu

Nchini India kuna makabila tofauti yanayoendeleza tamaduni ya mwanamke kuoa zaidi ya mume mmoja. Mfano makabila ya Toda na Kinnaur yanayopatikana maeneo ya milima kusini mwa India.

Tamaduni hiyo ilianza enzi za ‘Mahabharata’ ambapo bintimfalme Draupadi, mwanawe mfalme Drupada aliolewa na kaka watano waliojulikana kama Pandavas.

Pandavas na mke wao Draupadi waliishi katika milima ya Kinnaur. Wakaazi wa eneo hilo waliendeleza tamaduni hiyo wakiamini Pandavas walikuwa mababu zao.

Pandavas na mke wao Draupadi

Nchini Kenya, mwaka wa 2013 wanaume wawili waliweka makubaliano ya kumuuoa mke mmoja. Inadaiwa kuwa mwanamke huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wote wawili kwa zaidi ya miaka minne na inaonekana alikataa kuchagua kati yao, kwa hiyo Sylvester Mwendwa na Elijah Kimani wakaamua kukaa wote pamoja kwenye nyumba moja na kuwalea watoto watakaozaliwa kwenye uhusiano huo.

Nchini Rwanda, pacha wawili waliomuoa mke mmoja anayejulikana kama Marie Josiane, ni wengi wa furaha baada ya kupata habari kuwa mke wao anatarajia mtoto wao wa kwanza.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni nchini humo, wapenzi hao wanasema wanafurahia ndoa yao na familia yao, ingawaje jamii imeweka wazi kuwa hawafurahishwi na jisi wanavyoishi, wakisema ni kinyume na tamadauni zao.

Marie Josiane na waume zake

Kwa kuwa wanaharakati wa haki za kibinadamu hupigania usawa wa kijinsia, pengine utafika wakati ambapo ndoa kati ya mwanamke mmoja na wanaume wengi itakauwa ni jambo la kawaida.

Comments are closed