Mke wa Rais wa Marekani Jill Biden Jumapili alitembelea jamii zilizoathiriwa na ukame nchini Kenya na kutoa wito kwa mataifa tajiri kuchangia zaidi huku Pembe ya Afrika ikikabiliwa na hali mbaya zaidi ya ukame katika miongo kadhaa.
Biden alihitimisha ziara yake ya mataifa mawili barani Afrika kwa kutoa wito wa kuangaziwa zaidi juu ya ukame uliovunja rekodi ambao unatishia watu milioni 22 nchini Kenya, Somalia na Ethiopia na njaa.
Marekani imefadhili sehemu kubwa ya bajeti ya msaada kwa ajili ya maafa ambayo yameua mamilioni ya mifugo na kuharibu mazao.
“Hatuwezi kuwa sisi pekee. Inabidi nchi zingine zijiunge nasi katika juhudi hizi za kimataifa kusaidia watu hawa wa eneo hili,” alisema Biden katika kituo cha misaada huko Kajiado, kaunti kame kusini mwa Nairobi.
“Kwa bahati mbaya, unajua kuna vita huko Ukraine. Kuna tetemeko la ardhi huko Uturuki. Ninamaanisha kuna maslahi mengi yanayoshindana lakini ni wazi hapa … watu wana njaa.”
Biden alisikia kutoka kwa wazazi wanaotatizika kulisha watoto wao na jamii ambazo haziwezi kupata maji ya kutosha baada ya misimu mitano ya mvua kushindwa kufanyika.
Ukame ulikuwa lengo kuu la ziara ya Biden nchini Kenya, na mazungumzo mengine yakiangalia usalama wa chakula na kilimo katika hali ya hewa inayobadilika.
Biden pia alikutana na viongozi wa wanawake na vijana, akazuru vitongoji duni vya Kibera na kuweka shada la maua kwa waliouawa katika shambulio la bomu la ubalozi wa Marekani mjini Nairobi mwaka 1998.
Ziara yake nchini Kenya na kabla ya hapo Namibia inalenga kuendeleza Mkutano wa Viongozi wa Marekani na Afrika huko Washington mwishoni mwa mwaka jana ambapo Rais Joe Biden alisema nchi yake “imeingia” katika bara hilo lenye joto kali.