John Mnyika Aanza Kutoa Ushahidi Wa Utetezi Katika Kesi Ya Lissu

Shahidi wa pili wa upande wa utetezi, John Mnyika, ameanza kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam leo Ijumaa, Agosti 28, 2026.

John Mnyika Aanza Kutoa Ushahidi Wa Utetezi Katika Kesi Ya Lissu

Mnyika, mwenye umri wa miaka 46 na mkazi wa Goba, Dar es Salaam, ni Katibu Mkuu wa CHADEMA na ameitwa na Lissu kutoa ushahidi wa utetezi.Katika ushahidi wake, Mnyika ameeleza historia yake ndani ya CHADEMA, akieleza kuwa amekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho tangu mwaka 2019, baada ya kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya chama. Pia ametoa maelezo kuhusu majukumu ya Katibu Mkuu, muundo wa Sekretarieti ya chama pamoja na namna vikao vya ndani vinavyoandaliwa na kuitishwa.Sehemu kubwa ya ushahidi wa Mnyika imejikita katika mkutano wa CHADEMA uliofanyika Aprili 3, 2025 katika makao makuu ya chama Mikocheni, Dar es Salaam. Mnyika ameieleza Mahakama kuwa mkutano huo ulikuwa wa ndani wa chama, uliwahusisha watia nia wa uchaguzi wa mwaka 2025 pamoja na viongozi na waandishi wa habari.

Pia amesema yeye ndiye aliyekuwa nyuma ya wazo la mkutano huo, uliandaliwa kwa maelekezo yake na kusimamiwa na Sekretarieti aliyokuwa akiiongoza. Aidha, amesema Tundu Lissu, ambaye wakati huo alikuwa katika ziara ya Kanda ya Nyasa, hakushiriki kwa namna yoyote katika maandalizi ya mkutano huo.Haya ni baadhi ya maswali na majibu yaliyotolewa katika ushahidi wa Mnyika:LISSU: Sasa Shahidi umeeleza kwamba wewe ni mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam na kazi yako ni Katibu Mkuu wa Chadema. Naomba uwaeleze majaji umeshikilia kazi hii toka lini?MNYIKA: Tokea mwaka 2019.LISSU: Na uwaeleze Waheshimiwa Majaji kwamba kabla ya kuwa Katibu Mkuu ulikuwa nani?MNYIKA: Kabla ya kuwa Katibu Mkuu nilikuwa Mkurugenzi wa Vijana Taifa, kuanzia mwaka 2003, nafasi ambayo niliishikilia mpaka mwaka 2011. Wakati nashikilia nafasi hiyo, mwaka 2007 niliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, nafasi ambayo niliitumikia mpaka mwaka 2014. Wakati huohuo, kati ya mwaka 2009 mpaka 2011 nilishikilia nafasi ya Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ya Chadema. Na mwaka 2014 niliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, nafasi ambayo nilishikilia mpaka 2019 nilipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu.LISSU: Nafasi nyingine ya uongozi ya kichama, waeleze kama ipo.MNYIKA: Nilishawahi kuwa Mwenyekiti wa Kichama Mkoa wa Kinondoni.LISSU: Nafasi nyingine za chama kama ipo?MNYIKA: Nilipokuwa Mbunge wa Ubungo kuanzia mwaka 2010 mpaka 2015 na nilikuwa Mbunge wa Kibamba, Dar es Salaam, kati ya mwaka 2015 mpaka 2020.LISSU: Sasa Shahidi, nafasi ya Katibu Mkuu wa Chadema ni nafasi ya aina gani ya uongozi wa chama?MNYIKA: Nafasi ya Katibu Mkuu ni nafasi ya mtendaji wa chama ambaye ndiye Mwenyekiti wa Sekretarieti ya chama. Kwa nafasi hiyo, Katibu Mkuu ndiye msimamizi wa rasilimali, utawala, uendeshaji wa chama na Katibu Mkuu ndiye msimamizi mkuu wa utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya vikao vya juu vya Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Chama.LISSU: Sasa Shahidi, naomba uwaeleze Waheshimiwa Majaji kama chama chako huwa kinafanya vikao au mikutano ya chama na utaratibu wa kuitisha mikutano.MNYIKA: Chama huwa kina aina mbili za mikutano. Kuna mikutano ya ndani na kuna mikutano ya hadhara. Kwa upande wa mikutano ya ndani, ngazi husika na chombo husika ambacho ni Sekretarieti inakaa kikao. Kwa ngazi ya Taifa, chini ya Katibu Mkuu, inafanya maamuzi ya kufanya kikao husika na utaratibu wa maandalizi hayo.LISSU: Kama nakuelewa sawasawa kwamba kwa vikao vya ndani vya chama makao makuu, kazi ya kuandaa mikutano ya ndani ni kazi ya Sekretarieti. Sasa nani wajumbe wa hiyo Sekretarieti?MNYIKA: Ni Katibu Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wa Sekretarieti, Manaibu Katibu Wakuu wawili, mmoja wa Zanzibar na mwingine wa Tanzania Bara, Wakurugenzi wa Chama Taifa, wataalam na Katibu wa Sekretarieti na Makatibu wa Mabaraza ya Chama, Baraza la Wazee, Baraza la Vijana na Baraza la Wanawake.LISSU: Sasa Shahidi, katika wajumbe wote hao wa Sekretarieti ya Chama, waeleze Waheshimiwa Majaji kama Mwenyekiti wa Chama ni sehemu ya Sekretarieti ya Chama.MNYIKA: Mwenyekiti wa Chama si sehemu ya Sekretarieti ya Chama.LISSU: Na waeleze Waheshimiwa Majaji kama Mwenyekiti wa Chama anashiriki kwa namna yoyote ile kwenye vikao vya Sekretarieti ya Chama.MNYIKA: Mwenyekiti wa Chama hashiriki kwenye Sekretarieti ya Chama.LISSU: Sasa Shahidi, tupo Mahakamani leo kwa sababu ya kesi inayomkabili mimi na shtaka la kesi linasema kwamba mnamo tarehe 3 Aprili 2025 mimi niliitisha mkutano wa watia nia ya kugombea ubunge na nafasi mbalimbali zilizokuwa zinagombewa wakati huo. Na katika mkutano huo nilitengeneza nia ya kuvuruga uchaguzi huo. Sasa nataka ueleze kama una ufahamu wa mkutano huo.MNYIKA: Nina ufahamu wa mkutano huo, kwa sababu mkutano ambao wazo lilitoka kwangu, uliandaliwa kwa maelekezo yangu na ulisimamiwa na Sekretarieti ambayo niliisimamia vikao vya kupanga na kugawanya majukumu ya maandalizi. Niliidhinisha fedha za matumizi ya mkutano huo kama Account Officer na nilishiriki mkutano wenyewe.LISSU: Sasa Shahidi, kwenye ushahidi wako wa mwanzo ulisema kwamba kuna aina mbili za mikutano ya chama. Ulisema kuna mikutano ya hadhara na mikutano ya ndani. Waeleze Waheshimiwa Majaji huo mkutano wa tarehe 3 Aprili ulikuwa mkutano wa hadhara au wa ndani wa chama?MNYIKA: Ulikuwa mkutano wa ndani wa chama.LISSU: Huo mkutano ulikuwa unahusu nini na ulikuwa unawahusu watu gani?MNYIKA: Mkutano ulikuwa sehemu ya uhamasishaji au sehemu ya utekelezaji wa maadhimio ya Mkutano Mkuu wa Chama wa kutaka kufanyika kwa mabadiliko ya mageuzi ya kikatiba na ya kisheria kwa kuwezesha kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki chini ya kauli mbiu ya No Reforms No Elections na kwa tafsiri yetu ya Kiswahili, Bila mabadiliko hakuna uchaguzi.LISSU: Huo mkutano uliwahusu kina nani?MNYIKA: Mkutano huo uliwahusu waliokuwa na kusudio la kugombea kwenye uchaguzi wa mwaka 2025, maarufu kama watia nia wa uchaguzi.LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama kuna watu wengine nje ya hao watia nia mliowashirikisha kwenye mkutano huo.MNYIKA: Tuliwaalika viongozi wakuu wa chama na tuliwaalika waandishi wa habari.LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji, ukisema mlialika viongozi wakuu wa chama mnamaanisha kina nani?MNYIKA: Namaanisha Mwenyekiti wa Chama Taifa Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti Bara John Wagesa Heche, Makamu Mwenyekiti Zanzibar Said Said, na Katibu Mkuu ambaye ni sehemu ya Sekretarieti na Manaibu wake.LISSU: Katibu Mkuu, waeleze Waheshimiwa Majaji huo mkutano ulifanyikia wapi?MNYIKA: Ulifanyika makao makuu ya chama Mikocheni, Mtaa wa Daima, nyumba namba 31, katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu.LISSU: Sasa Shahidi, umesema kwamba mlialika vilevile vyombo vya habari. Ni vyombo vipi ambavyo unakumbuka?MNYIKA: Tulialika vyombo vingi vya habari na zoezi hilo lilifanywa na Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chama, na nilielekeza itolewe taarifa kwa umma ambalo lilitolewa tarehe 27 Machi 2025 lililosainiwa na Brenda Rupia, ambalo liliwaalika waandishi wa habari lakini pia liliutaarifu umma juu ya kikao hicho.LISSU: Sasa Shahidi, wakati wewe na Sekretarieti yako mnafanya yote hayo, Mwenyekiti wa Chama alikuwa wapi?MNYIKA: Wakati huo alikuwa kwenye ziara Kanda ya Nyasa kama sehemu ya Operesheni ya No Reforms No Elections.LISSU: Hiyo Kanda ya Nyasa ni kanda ya aina gani? Wafafanulie Majaji.MNYIKA: Inajumuisha mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa na Rukwa.LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji hiyo ziara ya Mwenyekiti Kanda ya Nyasa ilitumia muda gani?MNYIKA: Nakumbuka ilianza tarehe 23 Machi 2025 hadi kabla ya tarehe 3 Aprili 2025.LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji namna gani Mwenyekiti wa Chama alivyoshiriki kwenye maandalizi ya mkutano wa Aprili 3.MNYIKA: Mwenyekiti wa Chama hakushiriki kwa namna yoyote.LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji namna yoyote ile Mwenyekiti alishiriki kuwaalika watia nia au waandishi wa habari?MNYIKA: Mwenyekiti hakushiriki kuwaalika aidha watia nia au waandishi wa habari.LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji waandishi wa habari na vyombo vyao ambao unakumbuka kuhudhuria mkutano huo.MNYIKA: Nakumbuka Jambo TV, The Chanzo na Mwanzo TV.LISSU: Sasa Shahidi, baada ya ushahidi huo ambao umeutoa, hii tuhuma kwamba mimi Mwenyekiti wa Chama ndiye niliyeitisha huo mkutano wewe unaionaje?MNYIKA: Mheshimiwa Jaji, hiyo ni tuhuma ya uongo, tuhuma ya kubambikiza.LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji, wakati mnatuma mwaliko kwa hao waandishi wa habari, waeleze kama kulikuwa na maelekezo waje na nini.MNYIKA: Hakukuwa na maelekezo yoyote kwa waandishi wa habari waje na nini.LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji iwapo kulikuwa na maelekezo ya namna ya kutumia vifaa vyao.MNYIKA: Hakukuwa na maelekezo kwa waandishi wa habari juu ya namna ya kutumia vifaa vyao.LISSU: Sasa Shahidi, umesema mkutano ulihusisha hotuba fupi za viongozi na hotuba ndefu. Sasa lengo la kuwaita waandishi lilikuwa nini?MNYIKA: Lengo lilikuwa wao wachukue habari kufikisha kwa umma masuala yanayohusu masuala yetu ya mabadiliko ya kikatiba na kisheria na kuwezesha uchaguzi huru na haki chini ya kauli mbiu No Reforms No Elections.LISSU: Shahidi, umeileza Mahakama kwamba katika hotuba zilizotolewa, hotuba ya Mwenyekiti ilikuwa ndefu zaidi. Naomba ueleze Mahakama unamaanisha nini kusema hotuba ya Mwenyekiti ilikuwa ndefu zaidi?MNYIKA: Kwenye ile hotuba ilikuwa ya takribani saa 3. Katika muda huo, masaa 2 yalitumika kuzungumzwa na Mwenyekiti.

 

LISSU: Shahidi, waeleze Waheshimiwa Majaji mazungumzo ya Mwenyekiti yalihusu nini kama unakumbuka.

MNYIKA: Mwenyekiti alizungumzia historia ya madai ya kutaka mageuzi ya kikatiba kuwezesha uchaguzi huru na haki, kuanzia kabla na wakati wa Tume ya Rais ya kukusanya maoni maarufu kama Tume ya Nyalali. Inazungumzia namna mapendekezo ya Tume hiyo kutaka kufanyika mabadiliko ya kikatiba na kisheria ya kufanyika uchaguzi huru na haki na ilivyokataliwa na Serikali ya Chama kimoja ya Serikali ya CCM.

LISSU: Suala jingine?

MNYIKA: Akaendelea kuelezea juu ya madhara ya kutokufanyika kwa mabadiliko ya Katiba. Akaeleza maoni ya Kamati zilizoindwa kushughulikia masuala ya kikatiba, akataja Tume ya Kisanga, akataja Tume ya Jaji Mark Bomani na akaeleza kuhusu mchakato wa mabadiliko kati ya mwaka 2011 hadi 2014 ulioanzishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba maarufu kama Tume ya Warioba, namna CCM ilivyotumia wingi wake kwenye Bunge la Katiba kukwamisha mchakato huo.Akaeleza madhara ya kukosekana kwa mabadiliko hayo kwa uchaguzi mkuu wa 2015, uchaguzi wa vitongoji na vijiji wa mwaka 2019 na uamuzi wa Chadema kujiondoa kwenye uchaguzi huo baada ya wagombea wengi wa Chadema kuondolewa, na yaliyotokea katika uchaguzi wa 2020 ambapo yeye alikuwa mgombea Urais na baadhi ya wabunge ambao waligombea katika uchaguzi ule.Alizungumzia juu ya wagombea kuenguliwa kwa sababu za msingi na wengine kufungiwa kampeni, siku ya kura mawakala wa Chadema kuondolewa kwenye vituo vya kupigia kura, kura kuingizwa kwenye vituo vya kupigia kura zikiwa zimeishapigwa. Akaeleza hatua ambazo chama kimechukua mwaka 2020, wakati huo Mwenyekiti wa Chama akiwa Freeman Mbowe, za kudai mabadiliko ya Kikatiba na Tume Huru ya Uchaguzi.

Matokeo yake Mwenyekiti Mbowe akabambikiwa kesi ya Ugaidi na kukaa rumande kuanzia mwaka 2021 hadi 2022 na alipotoka kwa kesi yake kufutwa akakutana na Rais Samia na hatimaye kuanza kwa mazungumzo kati ya Chadema na CCM.Akaeleza kwamba katika mazungumzo hayo upande wa Chadema uliwasilisha kwa mazungumzo na maandishi mapendekezo ya maeneo ya marekebisho ya mabadiliko ya kikatiba kwa kuwezesha uchaguzi huru na haki na namna ambavyo baada ya mwaka mmoja ulivyojibu kwa mdomo na maandishi kukataa mapendekezo yote na marekebisho ya Katiba, kwa kuwezesha uchaguzi huru na haki na hatimaye mazungumzo kuvunjika.

LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji hayo mazungumzo na mapendekezo ya kikatiba yalikuwa yanahusu uchaguzi gani?

MNYIKA: Yalikuwa yanahusu uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa Urais, Ubunge na Madiwani wa mwaka 2025.

LISSU: Na waeleze Waheshimiwa Majaji ushiriki wako wewe mwenyewe katika mazungumzo hayo na Rais.

MNYIKA: Mimi nilikuwa sehemu ya timu ya Chadema ya watu 10 iliyokutana na huyo tarehe 22 Mei 2022 na katika timu yetu ya mazungumzo na Rais, mapendekezo ya kuamua mchakato wa Katiba yaliwasilishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wakati huo Freeman Mbowe.

LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji kilitokea kitu gani?

MNYIKA: Mapendekezo ya hoja nyingine 10, hoja mojawapo ikiwa ni marekebisho ya kisheria kuwezesha uchaguzi huru na haki wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu 2025, niliwasilisha mimi. Hayo mapendekezo yalikuwa ni mapendekezo sambamba kwamba iwapo mchakato wa Katiba Mpya ukichelewa, basi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025 kufanyike marekebisho katika maeneo mahususi ya Katiba tuliyoyapendekeza kwa kuwezesha uchaguzi huru na haki.

LISSU: Baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwenye kikao, mlichosema kitu gani kiliendelea?

MNYIKA: Rais aliahidi kwamba mchakato wa mazungumzo utaendelea na akaahidi kuunda timu ya watu watano wakiongozwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana, na kwa upande wetu alikuwepo Freeman Mbowe. Baadaye akaiunda ambapo nilikuwa sehemu ya watu watano.

LISSU: Waeleze Waheshimiwa Majaji mazungumzo kati ya timu hizo yaliendelea kwa muda gani na matokeo yake yalikuwa nini?

MNYIKA: Mazungumzo yalianza mwezi Juni 2022 mpaka tarehe 31 Mei 2023, upande wa CCM na Serikali ulipotujibu kwa mdomo na kwa maandishi kwamba hoja ya mchakato wa Katiba Mpya usubiri mpaka baada ya uchaguzi mkuu wa 2025. Pili, marekebisho yoyote ya Katiba yanayohusu uchaguzi, yanayogusa Katiba, hata kama ni marekebisho machache katika maeneo mahususi yatakayowezesha uchaguzi huru na matokeo ya urais kuhijiwa mahakamani na watumishi wa Tume wawe huru, ilimradi yanagusa Katiba, yasubiri wakati wa mchakato wa Katiba baada ya uchaguzi wa 2025.

Mnyika anakuwa shahidi wa pili wa utetezi baada ya Lissu ambaye ni shahidi wa kwanza wa utetezi kumaliza utetezi wake kwa kujitete mwenyewe

Kesi imeahirishwa mpaka Jumatatu Agost 31,2026 saa tatu asubuhi