Wakili wa kujitegemea Philip Mwakilima amelitaka Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya kuwafikisha Mahakamani Mwimbaji wa nyimbo za Injili Sifa Boniventure Bujune na mwandaaji wa mziki wa injili Ezekiea George wakihusishwa na tuhuma za uchochezi lakini bado wanashikiliwa na Polisi bila kupewa dhamana.
Akizungumza baada ya kuulizwa na wanahabari juu ya kinachomkabili mwimbaji Sifa Bujune mkazi wa Isyesye mkoani Mbeya Wakili Mwakilima, amesema mwimbaji huyo na mzalishaji wake wa mziki wanaendelea kushikiliwa kinyume cha sheria kwani ni zaidi ya saa 24 hawajafikishwa Mahakamani wala kupewa dhamana.
Wakili huyo amelitaka jeshi la Polisi kuwaachia huru wawili hao akidai wametoa maoni yao kupitia njia ya uimbaji hivyo maoni yao yalipaswa kutazamwa kwa maslahi ya Taifa badala ya kuwashughulikia kama wakosaji.
Mwakilima anasema ni haki ya kila mtu kutoa maoni juu ya nchi yake bila kuvunja sheria za nchi na kwamba.
Modester Peter Mwailenge ni mwana Familia ya waliokamatwa na Polisi wakituhumiwa kuimba wimbo wenye maudhui ya uchochezi anaeleza kushangazwa na kitendo cha Polisi kuingilia maswala ya maudhui kwenye nyimbo badala ya Baraza la sanaa Tanzania BASATA huku ndugu wengine nao wakushangaa kushikiliwa ndugu hao kwa siku kadhaa sasa bila kuwafikisha Mahakamani.
Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya linaendelea kumshikilia binti Sifa Boniventure na Ezekia George wakituhumiwa kwa masuala ya uchochezi kupitia wimbo uliosambazwa kwenye mtandao wa YouTube ukidaiwa kuwa na maudhui ya uchochezi wimbo ambao unatajwa na baadhi ya watu kuwa umegusa maeneo nyeti yanayoonekana kupigiwa kelele ikiwemo ugumu wa maisha, mgogoro wa wananchi wa Ngorongoro na Liliondo mkoani Arusha kati yao na Serikali sanjari na suala la bandari ambalo mkataba wake unaendelea kugomewa na wananchi na wadau mbalimbali nchini kwa madai kuwa mkataba huo sio rafiki kwa mtanzania.