Kampuni ya Amazon huenda ikasitisha ujenzi wa makao makuu yake mjini Cape Town

Kampuni kubwa ya reja reja ya mtandaoni ya Amazon inaweza kujiondoa katika makubaliano ya kuunda makao makuu yake ya Afrika mjini Cape Town, ikiwa pingamizi la wanaharakati wa kiasili litaruhusiwa kuendelea, mahakama ya Cape Town ilisikiza Alhamisi.

Ujenzi tayari unaendelea kwa makao makuu ya Afrika ya Amazon yatakayogharimu randi bilioni nne ikiwa ni dola milioni 262 au euro milioni 231.

Ujenzi wa makao hayo makuu unafanyika kwenye ardhi ambayo jamii za Khoisan huchukulia kuwa takatifu, ikiwa kama kumbukumbu yao ya vita dhidi ya wakoloni wa Uropa mnamo 1510.

Vikundi kadhaa vya Khoisan vimeunga mkono mradi huo, baada ya waendelezaji kukubali kujenga kituo cha urithi, utamaduni na kituo cha habari ambacho kitaendeshwa na vikundi vya kiasili.

Lakini Baraza la Jadi la Goringhaicona Khoi Khoin na jumuiya ya kitongoji wameiomba Mahakama Kuu ya Cape Magharibi kusitisha ujenzi huo.

Wakili wa waendelezaji hao, Liesbeek Leisure Property Trust, aliiambia mahakama kwamba Amazon imeashiria kuwa itajiondoa katika mradi huo iwapo ujenzi wa makao makuu utaendelea kucheleweshwa.

“Amazon imeonyesha kuwa haitavumilia kwa mradi wao kucheleshwa zaidi ya ulivyocheleshwa,” wakili Sean Rosenberg aliiambia mahakama.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba mradi huu hautaendelea, kutokana na kile ambacho kimetokea hadi sasa,”

Amazon haijatajwa katika kesi hiyo. Kesi inatarajiwa kukamilika Ijumaa.

Hadi miaka miwili iliyopita, ardhi hiyo ilikuwa na uwanja wa gofu.

Mamlaka ya jiji mwaka jana iliidhinisha ujenzi wa jengo la ghorofa tisa la biashara na makazi kwenye uwanja ambao Amazon walitarajia kuweka makao yake makuu.

Jamii ya Khoisan ambao walikuwa wawindaji na wakusanyaji waliojulikana zaidi kama Bushmen, waliteseka sana chini ya ukoloni na ubaguzi wa rangi.

Wengi katika jamii hiyo wanasema bado wanavumilia ubaguzi wa kijamii na hawapati fursa za kiuchumi, na kuwa maisha yao ya awali hayazingatiwi.