Watu mjini Ontario Canada wana fursa ya kufanya oda na kununua bangi kupitia programu ya Uber Eats baada ya huduma ya utoaji wa chakula kuingia katika ushirikiano na muuzaji halali wa bangi.
“Wateja wanaweza kuagiza bangi kutoka kwa duka la Tokyo Smoke’s flower collection and unique accessories kutoka Tokyo Japan kwenye programu ya Uber na kuchukua oda yao kutoka kwa matawi ya duka hilo mjini Ontario,” kampuni hizo zilisema katika taarifa yake kutangaza ushirikiano huo ambao ni wa kwanza wa aina yake.
Wanaahidi kwamba maagizo yatakuwa tayari ndani ya saa moja baada ya kuagiza. Mtu yeyote anayetoa agizo lazima athibitishe umri wake halali kwanza.
Kampuni ya Tokyo Smokes ina matawi 56 mjini Ontario ikiwemo matawi mengine 13 mjini Toronto.
Uber Eats na Tokyo Smoke zinasisitiza kwamba ushirikiano wao utachangia katika vita dhidi ya uuzaji haramu wa bangi, ambao kulingana na takwimu rasmi, unachangia zaidi ya 40% ya mauzo yote ya bangi yasiyo ya matibabu nchini Canada.
Uber Eats ina mipango mikubwa zaidi
“Sheria za bangi za Canada zitakapobadilika na kujumuisha biashara kama vile Uber Eats zitasaidia kupunguza ajali za barabarani unaosababishwa na watumizi wa bangi,” ilisema taarifa hiyo.
Utafiti wa hivi majuzi kutoka kwa kampuni ya ushauri ya Public First yenye makao yake nchini Uingereza unaonyesha kuwa 14% ya watumiaji wa bangi huendesha gari ndani ya saa mbili baada ya kutumia bangi.
Chini ya sheria za Canada, ingawa matumizi ya bangi yamekuwa halali tangu 2018, bado ni haramu kuiwasilisha.
Soko la bangi la Canada linakadiriwa kuendelea kukua katika miaka ijayo na kampuni ya utafiti wa tasnia ya BDS Analytics inatarajia mauzo kuongezeka hadi dola bilioni saba ($6.7bn) ifikapo mwaka wa 2026.
Mamlaka ya Ontario iliruhusu uwasilishaji na uchukuzi wa bangi wakati wa janga la UVIKO 19. Mnamo Oktoba, sheria ilipendekezwa kufanya mpango huu kuwa wa kudumu, lakini bado haujapitishwa.