Serial killer, inamaanisha mtu ambaye amewaua watu wengi katika kipindi cha muda fulani.
Kulingana na wanasaikolojia, serial killer ni mtu ambaye amewaua watu watatu na zaidi, wengi wa wauaji hao wakijihusisha na vitendo vya ngono na waathiriwa wao.
Ofisi ya Upelelezi FBI inasema kwamba wauaji huua kwasababu ya hasira waliyonayo kwa jamii, kutaka kufaidika kifedha, na kutafuta umaarufu.
Katika wiki za hivi karibuni, Kenya imeshuhudia kisa cha mtu aliyekiri kuwaua watoto 14 na baadae kutoroka jela alikokuwa amezuiliwa na kukimbilia kijiji chake magharibi mwa Kenya alikouawa na majirani.
Kisa cha Masten Milimu Wanjala mwenya umri wa miaka 20 kiliwashangaza wengi si tu Kenya bali pia watu katika mataifa mengine barani.
Wanjala alikiri kuwateka watoto kumi na wanne katika kipindi tofauti na kuwaua, wengine akiwafyonza damu baada ya kuwaua.
Inasemekana kuwa Wanjala, alijifanya kuwa kocha wa mpira na kuwavutia watoto waliopenda soka. Alimuua mtoto wa kwanza akiwa na umri wa miaka 16.
Muuaji mwingine kutoka Kenya ambaye aliwatia wengi hofu ni Philip Onyancha.
Philip Onyancha aligonga vichwa vya habari mwaka wa 2010 baada ya kukiri kuwaua wanawake 17, katika mahojiano na majasusi Onyancha alidai kuwa kueelekezwa na kiongozi wa dhehebu fulani kuwa anatakiwa kunywa damu ya watu 100.
“Lengo langu ilikuwa niwauwe wanawake 100 na kunywa damu zao, ila nilifaulu kuwaua 17 pekee, hivyo hesabu yangu haijakamilika,” alisema Onyancha alipohojiwa.
Mahakama ya Nairobi ilimuachilia huru kwa mauji ya Chepngetich Misoi yaliyofanyika mnano mwaka wa 2008.
Geoffrey Matheri ni muuaji mwingine ambaye aliwatia hofu wakenya baada ya wanawake wawili kuokolewa kutoka nyumba walikokuwa wamezuiliwa na Matheri.
Inasemekana kuwa Matheri alikuwa akiwafyonza damu watu aliowatekwa nyara wakiwa bado hai. Alihukumiwa kwa makosa ya mauaji na mahakama moja nchini Kenya, alikiri kuwa baada ya kuwaua waathiriwa alikuwa akipeleka damu yao kwa kasisi mmoja mjini Nairobi.
Kando na wauaji hao kutoka Kenya, kumekuwa na wauaji wengine wengi kutoka mataifa tofauti duniani, ikiwemo Afrika Kusini, Misri, Pakistan, India, China na Amerika.
Katika historia, kumekuwa na wauaji ambao wameua zaidi ya watu 300. Katika rekodi muuaji aliyewahi kuwaua watu wengi zaidi ni Luis Garavito kutoka mataifa ya Amerika kusini ya Colombia na Ecuador.
Inasemekana kuwa Luis Garavito aliwaua kati ya watu 172 hadi 300, wengi wao ikiwa ni wavulana wa kati ya umri wa miaka 8 hadi 16 katika kipindi cha miaka 7 kati ya mwaka wa 1992 hadi 1999.
Garavito anatuhumiwa kuwaua tarkriban watoto 300, wengi wao ambao walikuwa watoto wakurandaranda mitaani. Alihukumiwa kifungo cha miaka 1,853 gerezani ila baada ya kuwasaidia majasusi kupata miili ya waathiriwa hukumu yake ilipunguzwa hadi miaka 22, na anatarajiwa kuachiwa huru mwaka wa 2023.
Kutoka Afrika kusini, muuaji kwa jina Moses Sithole anasemekana kuwaua watu 70 kati ya mwaka 1994 hadi 1995.
Sithole alijifanya kuwa mfanyabiashara na kuwavutia wanawake waliokuwa wakitafuta ajira. Sithole baadae aliwabaka, kuwatesa na kuwaua wanawake hao. Alihukumiwa kifungo cha miaka 2410 gerezani bila uwepo wa msamaha.
Muuaji mwingine aliyegonga vichwa vya habari hususan nchini Marekani ni Ted Bundy.
Bundy anasemekana kuwaua takriban watu 36 hadi 100 katika kipindi cha mwaka wa 1974 hadi 1978, alikiri kuwaua wanawake 36. Bundy alifahamika pia kwa kutoroka jela mara mbili na kuwaua wanawake wengi kutoka mtaa mmoja alikowateka nyara. Alipewa adhabu ya kifo na kuuawa kwa umeme.