Watafiti katika Tume ya Umoja wa Ulaya walionya siku ya Jumatatu kwamba karibu nusu ya eneo la Umoja wa Ulaya kwa sasa liko katika hatari ya ukame, huku Ulaya ya Kusini-magharibi ikikauka kutokana na wimbi la joto.
Katika ripoti ya mwezi Julai, Kituo cha Utafiti cha Pamoja cha Tume ya Ulaya kilisema kuwa asilimia 46 ya eneo la Umoja wa Ulaya limekabiliwa na ukame wa kiwango cha juu, huku asilimia 11 ikiwa katika kiwango cha tahadhari, mimea ikiwa tayari inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.
Italia ndiyo iliyoathirika zaidi, huku bonde la Mto Po kaskazini mwa nchi likikabiliwa na kiwango cha juu zaidi cha ukame, ilisema EU.
Nchini Uhispania, ujazo wa hifadhi ya maji kwa sasa uko chini kwa asilimia 31 kuliko wastani wa miaka 10, ripoti ilisema, wakati nchini Ureno, maji ya kuzalisha nishati ya umeme wa maji ni nusu ya wastani ya miaka saba iliyopita.
Watafiti wa EU pia walionya kuwa uhaba wa maji na joto kali vinasababisha mazao kupungua Ufaransa, Romania, Uhispania, Ureno na Italia.
Utabiri wa hali ya hewa unatabiri hayo huku ikiongeza kuwa kuna ‘hali mbaya sana’ ambayo itazidisha athari kwenye kilimo, nishati na usambazaji wa maji.