Takriban wiki moja baada ya marubani wa shirika la ndege la Kenya Airways kurejea kazini, kampuni hiyo imetangaza kuanza safari za moja kwa moja kati ya Mombasa na Dubai mnamo disemba 15, 2022.
Shirika hilo linatazamiwa kuendesha safari hiyo mara nne kwa wiki kwa ndege yake aina ya Boeing 737-800.
Shirika hilo la kitaifa linasema kuanzishwa kwa safari hiyo kunatokana na mahitaji kutoka sokoni.
Safari za ndege za moja kwa moja kati ya Mombasa na Dubai zinatarajiwa kuupa Jiji la pwani ufikiaji wa moja kwa moja kwenye soko la Mashariki ya kati.
“Kuanzishwa kwa njia hii ni muhimu nay a kimkakati kwani itafungua eneo la pwani ya Kenya, kukuza sekta ya utalii na ukarimu na pia kuchochea biashara katika Jiji la pwani,” alisema Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja wa Kenya Airways Julius Thairu.
Ndege hiyo inatarajiwa kutoka Nairobi na itatumika kuongeza masafa ya KQ hadi Dubai hadi mara 14 kwa wiki.
KG itaanza safari hiyo ya ndege kutoka Mombasa siku ya Jumatatu, Jumanne, Alhamisi na Jumamosi na kufanya safari za kurudi kutoka Dubai Jumanne, Jumatano, Ijumaa na Jumapili.
Kando na sekta ya utalii, safari hizo mpya za ndege zimewekwa kuwanufaisha wafanyibiashara watakuwa na uwezo wa kubeba mizigo kwenye ndege.