Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ameamuru kukamatwa kwa mkuu wa shule ya upili ya Tot baada ya basi la shule hiyo kuvamiwa na majambazi waliokuwa wamejihami.
Dereva wa basi alifariki papo hapo huku wanafunzi 13 na walimu 2 wakipata majeraha baada ya majambazi hao kumiminia risasi basi lao katika eneo la Kerio Valley.
Kulingana na Matiang’i, mkuu wa shule atakamatwa kwa kuruhusu basi la shule kuwa barabarani mwendo wa saa kumi na mbili na nusu jioni jambo ambalo ni kinyume na sheria na sera ya nchi kuhusu muda wa mabasi kuwa barabarani na wanafunzi.
Kisa hicho kilitokea Alhamisi usiku mwendo wa saa 4 usiku katika barabara ya Arror-Mogil karibu na Tot katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Walimu na wanafunzi hao walikuwa wakitoka katika safari ya kimasomo katika msafara wa mabasi matatu ya Shule ya Tot Day, Shule ya Kerio Valley na shule ya Mogil wakati shambulio hilo lilipotokea.
Wanakijiji walikimbilia eneo la tukio kuwaokoa majeruhi waliokimbizwa katika hospitali ya misheni ya Kapsowar kwa matibabu.
Agizo la kukamatwa kwa mkuu wa shule hata hivyo limewakasirisha Wakenya ambao walijiuliza ikiwa hiyo ndiyo suluhu ya mashambulizi ya ujambazi ambayo yametikisa Kerio valley kwa muda mrefu.