Bingwa mara mbili wa mbio za Olimpiki Faith Kipyegon aliipa Kenya medali yake ya kwanza ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwa wanawake katika Riadha za Dunia zinazoendelea huko Oregon.
Kipyegon alitumia muda wa 3:52.96 kuhifadhi taji aliloshinda mjini Doha mwaka wa 2019 huku Muethiopia Gudaf Tsegay akitwaa medali ya fedha kwa muda wa 3:54.52.
Laura Muir wa Uingereza alipata medali ya shaba kwa muda wa 3:55.26.
Muda alioweka Kipyegon ni wa 10 kwa kasi zaidi kuwahi kutokea na ni mara ya 2 kukimbia kwa kasi zaidi nchini Marekani, baada ya muda wake wa 3:52.59 katika Prefontaine Meet ya 2022.
Bingwa huyo wa Olimpiki mara mbili sasa ameshinda taji la dunia mara mbili akitwaa tena taji alilopoteza mwaka wa 2019 kwa Sifan Hassan wa Uholanzi ambaye hakushiriki mbio za mita 1500 mwaka huu.
Kipyegon amekuwa mwanamke wa kwanza kabisa kushinda medali nne za Ubingwa wa Dunia katika mbio za 1500m.
Mnamo 2015 na 2019 alishinda fedha, na sasa mataji mawili ya mwaka 2017 na 2022.