Kenya: Gavana Joho ajiondoa kuwania Urais

Raila Odinga, Ali Hassan Joho na Wycliffe Oparanya

Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho na mwenzake wa Kakamega Wycliffe Oparanya wametupilia mbali azma yao ya urais na kumuunga mkono kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Wakizungumza wakati wa Kongamano la Kitaifa la Uongozi la ODM katika Ukumbi wa Bomas of Kenya siku ya Ijumaa ambapo Odinga aliidhinishwa kuwa mgombeaji urais wa ODM, magavana hao wawili walisema waziri mkuu huyo wa zamani ndiye anayeweza kubeba bendera ya ODM katika uchaguzi wa Agosti 9.

“Natangaza rasmi mbele ya NGC kwamba najiondoa kutoka kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya ODM na sasa namuidhinisha Raila Odinga kama mgombeaji wangu wa urais,” Joho alisema.

https://www.youtube.com/watch?v=exys2xgPXyc

Gavana Joho alimsifu Odinga kwa tajriba na ukomavu wake katika siasa akimtaja kama mshauri aliyemsaidia kukomaa katika siasa.

“Umekuwa mshauri wangu wa kisiasa tangu 2004 na hakuna vile  nitashindana nawe,”Joho alisema.

Joho na Oparanya hapo awali walitangaza nia zao kuwania kiti cha rais lakini tangu wakati huo wamekuwa wakiunga mkono muungano wa Azimio la Umoja unaoongozwa na Raila.