Hatimaye tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC imekubali kufuata agizo la mahakama ya upeo na kufungua sava zote ili wahusika waingie kwenye mitambo hiyo, hatua ambayo imepisha zoezi la uhakiki kuanza.
Kupitia ukurasa wao wa mitandao ya kijamii, IEBC imeandika kuwa imefungua sava zote jinsi mahakama ilivyokuwa imeajiza na zoezi la uhakiki linaendelea.
Awali kulishuhudiwa hali ya kutoelewana katika makao makuu ya tume ya IEBC jijini Nairobi baada ya tume hiyo kudinda kufungua sava zote jnisi mahakama ya juu ilivyoamrisha
Mahakama ya upeo ilimpa Raila Odinga nafasi ya kuona teknolojia iliyotumika katika kusambaza matokeo katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha matokeo ya urais eneo la Bomas Nairobi.
Kulingana na wakili James Orengo, tume ya IEBC hata hivyo ilikuwa imepeana nafasi ya kutazama sava moja pekee kati ya nane zilizotumika.
“Tumepewa nafasi finyu ya kukagua mitambo hiyo ndani ya sava moja tu. Hii ni licha ya mahakama kubaini kuwa IEBC ina sava nane.” Alisema Orengo.
Orengo alikuwa ameiambia jopo la majaji saba wakiongozwa na jaji mkuu Martha Koome kwamba walikuwa wameandika waraka kwa msajili mkuu wa idara ya mahakama Anne Amadi kuhusu suala hilo na kuitaka mahaka hiyo kuingilia kati.
“Tumeandika barua kwa idara ya mahakama ili korti iingilie kati katika kutatua utata huu” alisema Orengo
“Tumefahamu hayo na tunashughulikia jambo hilo. Tunachojua ni kwamba tulipotoka hapa zoezi hilo lilikuwa limeanza, kulikuwa mwafaka kuhusu jinsi ya kuingia katika sava ambayo ilikuwa imepeanwa,” alisema jaji Isaac Lenaola.
Siku ya Jumanne IEBC iliamrishwa kufungua sava iliyotumika kupokea fomu ya 34C katika kitovu cha IEBC wakati wa kikao cha kwanza cha kesi hiyo ya urais.
Suala la kufungua mitambo linawakumbusha Wakenya kuhusu mwaka wa 2017 wakati ambao kesi ya uchaguzi wa urais ilikuwa katika mahakama hiyo na suala la sava likawa kuu.
Mahakama ilisema IEBC wakati huo ilifanya kosa kukosa kufungua sava zake kwa walalamikaji mahakamani.