Serikali ya Kenya inasema haina nia ya kuzima mitandao ya kijamii wakati wa uchaguzi wa Agosti 9
Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alisisitiza msimamo huo alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa warsha ya mikakati ya Kitaifa ya usalama wa mtandao 2022-2026.
Alitaja kitendo hicho kuwa cha kurudisha nyuma maendeleo ya nchi katika uhuru wa kujieleza.
“Hatutashiriki katika vitendo vya kurudi nyuma kama vile kubana matumizi ya mtandao wakati wa uchaguzi.”
Waziri huyo, ambaye alikiri kwamba kulikuwa na ongezeko la habari za uwongo na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo hayajawahi kushuhudiwa, alisema mtandao umekuwa suala gumu kwa polisi, huku vyombo vya usalama vikishughulikia kesi za ndani na nje.
Matiang’i pia alisisitiza haja ya kuwekeza katika usalama wa mtandao, na kuongeza mkakati uliozinduliwa utasaidia katika vita dhidi ya uhalifu mtandaoni.
“Tunapokaribia uchaguzi tutakuwa tukikabiliana na ongezeko la visa vya habari ghushi miongoni mwa mambo mengine. Kama sekta ya usalama inayojumuisha Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Kurugenzi ya Uchunguzi wa Jinai (DCI), na Huduma za Kitaifa za Ujasusi (NIS), tumejenga uwezo wa kimataifa,” akadokeza.
Alisema Kenya ni nchi ya kidemokrasia na serikali haiwezi kujihusisha na vitendo vya kuvurga demokrasia kama vile kufunga mtandao na kurudisha nyuma mafanikio ya kikatiba.
Matiang’i pia aliwahakikishia Wakenya kuwa serikali itashughulikia masuala ya propaganda miongoni mwa wanasiasa.
Hii ni mara ya pili katika mwaka mmoja ambapo Matiang’i anathibitisha dhamira ya serikali kutobana uhuru wa kujieleza mtandaoni, “Mitandao ya kijamii ya Kenya haitazimwa kutokana na matamshi ya chuki.
Hata hivyo, tutakuwa wakatili sana kwa wale ambao watahatarisha uhuru wa wengine. Hatutasita au kutishwa na shinikizo au malalamiko kutoka kwa mtu yeyote. Tutailinda Kenya,” akasema.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kawaida hupeperusha matokeo ya uchaguzi kwenye tovuti yake yanapojitokeza, zoezi ambalo linahitaji mtandao.