Idadi ya wanawake waliochaguliwa magavana nchini Kenya imeongezeka maradufu kutoka watatu mwaka 2017 hadi saba mwaka huu wa 2022.
Hii ina maana kuwa serikali inayokuja itakuwa na magavana saba wanawake. Hali hii inatarajia kupiga jeki juhudi za kupitisha mswaada wa theluthi moja wanawake ambayo imepingwa na wanaume kwa muda mrefu.
Wapate kujua magavana wateule wanawake saba hawa
Kawira Mwangaza gavana mteule Meru
Aliyekuwa mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Meru, Kawira Mwangaza amefanikiwa kuwabwaga gavana wa sasa Kiraitu Murungi na Seneta wa sasa Mithika Linturi.
Mwangaza aliwania kama mgombea huru na alijipatia kura 209,148 huku Linturi akiwa wa pili na kura 183,859 na gavana Kiraitu akawa wa mwisho kwa kura 110,814.
Ann Mumbi Waiguru gavana mteule Kirinyaga
Waiguru amehifadhi kiti chake baada ya kujizolea kura 113,099 na kumpiku mpinzani wake wa karibu ambaye ndiye mwakilishi wa wanawake anayeodoka wa kaunti hiyo Purity Ngirici ambaye alipata kura 105,677.
Mnamo mwaka wa 2017, Waiguru alihudumu kama waziri wa kwanza wa ugatuzi na mipango katika serikali ya rais Uhuru Kenyatta.
Pia alihudumu kama naibu mwenyekiti wa kwanza wa bazara la magavana kati ya mwaka wa 2017 na 2019.
Susana Kihika gavana mteule Nakuru
Susan Kihika ameandika historia kama mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kama gavana katika kaunti ambayo imeandika historia nyingine ya kipekee ya kuwachagua wanawake wengi katika nafasi za uongozi.
Kihika ambaye aliwania kupitia chama cha naibu wa rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA) alipata kura 440,707 na kumshinda gavana anayeondoka Lee Kinyanjui ambaye alipata kura 325,623.
Mwaka 2013 aligombea ubunge eneo la Bahati japo alishindwa.
Kihika alifanikiwa kuwashinda wawaniaji saba katika nafasi yua uspika wa kaunti hiyo ya Nakuru ambako alihudumu kwa miaka mitano.
Mwaka 2017 aliingia bungeni kwa mara ya kwanza kama seneta wa Nakuru alipojipatia kura 637,700.
Gladys Wanga gavana mteule wa Homa Bay
Gladys Wanga pia ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa gavana kaunti ya Homa Bay.
Wanga ambaye amekuwa gavana kupitia tiketi ya chama cha mgombea urais Raila Odinga cha Orange Democratic Movement (ODM), alipata kura 244,559 dhidi ya mpinzani wake Evans Kidero ambaye alikuwa gavana wa kwanza wa jimbo la Nairobi aliyepata kura 154,182.
Mwaka 2017, Wanga alichaguliwa kuwa mwakilishi wa wanawake kaunti hiyo hiyo na baadaye kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya bajeti katika bunge la kitaifa.
Cecily Mbarire gavana mteule Embu
Cecily Mbarire amechaguliwa kuwa gavana wa Embu baada ya kupata kura 108,610 kupitia chama cha UDA.
Mbarire amewashinda seneta wa kaunti hiyo anayeondoka Lenny Kivuti wa chama cha DEP ambaye amepata kura 105,246 na gavana anayeondoka Martin Wambora ambaye amepata kura 110,814.
Mbarire aliteuliwa kuwa mbunge mteule katika akiwakalisha mahitaki maalum katika bunge la kitaifa na aliwai kuwa mbunge wa Runyenjes.
Mwaka wa 2007, aliwania kupitia chama cha PNU na mwaka 2013 akahifadhi kiti chake kupitia chama cha The National Alliance (TNA), kabla ya hapo alikuwa ameteuliwa na chama cha Narc.
Wavinya Ndeti gavana mteule wa Machakos
Wavinya Ndeti anakuwa gavana wa kwanza mwanamke baada ya kuwania kiti hicho kwa miaka miwili mfululizo.
Alipita na kura 226,609 katika mchuano mkali na kumshinda aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma katika Ofisi ya Rais, Nzioka Waita ambaye alipata kura 129,189.
Wavinya alijiuzulu kama waziri msaidizi mapema mwaka huu ili kuwania kiti hicho.
Mwaka wa 2007, Wavinya alichaguliwa kama mbunge wa Kathiani ndani ya chama cha Uzalendo.
Baada ya ushindi wake Wavinya anakuwa mwanamke wa pekee kuwahi kuwakilisha eneo bunge tangu Kenya ijinyakulie uhuru.
Fatuma Achani gavana mteule wa Kwale
Fatuma Achani wa chama cha UDA ameshinda kiti cha ugavana kaunti ya Kwale kwa kupata kura 59,674 na kumshinda Hamadi Boga wa chama cha ODM ambaye alipata kura 53, 972.
Achani ambaye ni wakili amekuwa naibu wa gavana wa kaunti hiyo. Fatuma Achani ameweka historia kwa kuwa gavana wa kwanza mwanamke katika kaunti hiyo ya Kwale na vilevile gavana wa kwanza mwanamke kutoka eneo la Pwani.