Vita vya kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto vilionekana wazi wakati wa sherehe za siku ya Madaraka.
Rais Uhuru Kenyatta alichukua uongozi wa sherehe hizo baada ya onyesho la kijeshi na burudani ya kusherehekea miaka 59 ya madaraka ya Kenya
Mara tu baada ya burudani kutoka kwa wasanii kama vile Iyanni, Trio Mio na Femi One, Rais Kenyatta aliwatunukia tuzo baadhi ya wakenya.
Baada ya kutoa tuzo, Rais Uhuru Kenyatta aliendela kusoma hotuba yake.
Naibu Rais William Ruto alipuuzwa na Kenyatta katika itifaki iliyozoeleka ambapo yeye ndie angemwalika mgeni rasmi Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio kuhutubia taifa.
Badala yake, mara tu Rais Kenyatta alipokamilisha hotuba yake alimwalika Rais Bio kuhutubia wakenya.
Hii ilikuwa mara ya kwanza tangu Uhuru Kenyatta kuingia madarakani 2013 kwake yeye kuvunja itifaki.
Hii imechukuliwa na Wakenya wengi kuwa kilele cha uhasimu kati ya Dkt Ruto na Rais Kenyatta, ambaye hivi majuzi, kwenye hafla ya maombi ya kitaifa alikwepa kushiriki meza moja.
Kenyatta hata hivyo amewakosesha wakenya nafasi ya kumsikiliza Naibu Rais katika sikukuu yake ya mwisho ya Madaraka kama Naibu Rais.
Hapo awali, Rais Kenyatta alikosa kumwalika naibu wake William Ruto kwenye hafla fupi katika Ikulu kabla ya hotuba yake kwa taifa kuadhimisha Siku ya 59 ya Madaraka katika bustani ya Uhuru Nairobi.
Badala yake, Naibu Rais aliachwa kumkaribisha Rais wa Sierra Leone Maada Bio katika bustani ya Uhuru, huku Rais Kenyatta akicheza na kwaya ya Ikulu baada ya kukutana na Baraza lake lote la Mawaziri.
Msemaji wa Ruto, Emmanuel Talam alisema kuwa Naibu Rais hakualikwa Ikulu.
Katika ukumbi wa sherehe za Madaraka Day kulikuwa na kinara wa ODM Raila Odinga na mgombea mwenza Martha Karua, ambao waliandamana na wanasiasa wengine.
Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka walihudhuria sherehe hizo.
Hili litakuwa tukio maalum kwa rais, ikiwa hii ni sherehe yake ya mwisho kama rais kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.
Uhuru, ambaye pia ni mlezi katika Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya amemtaja Raila kama mtu bora zaidi kumrithi, kwa kile naibu wake Ruto amekitaja kuwa usaliti.