Jaji Mkuu Martha Koome anamtaka Rais Uhuru Kenyatta ang’olewe madarakani kwa kukosa kuwateua majaji sita waliopendekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).
Kulingana na CJ Koome, suluhisho la kukataa kwa Rais Kenyatta kuwateua majaji sita kati ya 40 waliopendekezwa ni kuondolewa kwake madarakani.
Koome anapendekezwa kuwa mahakama itoe tamko kwamba Rais anakiuka Ibara ya 3(1) na 166(1)(b) ya Katiba. Tamko kwamba suluhisho sahihi la ukiukwaji wa Ibara ya 3(1) na 166(1)(b) ya Katiba ni kushtakiwa kwa Rais au amri nyingine yoyote ambayo inahakikisha uwajibikaji wa moja kwa moja wa Rais.
Rais Kenyatta alikataa kuwateua majaji sita akinukuu ripoti ya Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) ambayo ilikuwa imefichua kwamba wote sita walikuwa hawastahili.
Majaji hao sita ni pamoja na George Odunga, Prof Joel Ngugi, Weldon Korir, Aggrey Muchelule, Hakimu Mkuu Evans Makori na naibu msajili wa Mahakama Kuu Judith Omange.
Waliteuliwa na JSC mnamo Julai 2019 pamoja na wengine 35, lakini mmoja wao, Harrison Okeche, alifariki wakati wa mvutano huo.
Mwenyekiti wa JSC wakati huo alikuwa Jaji Mkuu David Maraga, ambaye aliondoka afisini Januari 2021. Rais Kenyatta aliteua majaji 34 mnamo Juni 4, 2021, na kuwakataa sita hao kutokana na madai ya masuala ya uadilifu.
Mahakama ya majaji watatu Oktoba 21, 2021, ilitoa uamuzi wa kesi iliyofunguliwa na kikundi cha ushawishi cha Katiba Institute, ikimuagiza Rais kuwateua majaji hao sita ndani ya siku 14 kuanzia siku ya hukumu hiyo.
Katiba katika Ibara ya 145—juu ya kuondolewa kwa Rais kwa kushtakiwa—inaeleza kwamba hoja ya kumshtaki iliyowasilishwa na mjumbe wa Bunge lazima iungwe mkono na angalau theluthi moja ya wajumbe wote 232.
CJ Koome anadai kuwa Rais amekiuka Ibara ya 3(1) inayosema “kila mtu ana wajibu wa kuiheshimu, kuilinda na kuitetea Katiba hii”.
Kipengele kingine anachodai kuwa Bw Kenyatta amekiuka ni Kifungu cha 166(1)(b), kinachosema kuwa “Rais atateua majaji wengine wote, kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Mahakama.”
Katiba inatoa njia mbili za kumuondoa Rais madarakani.
Kwanza kupitia mashtaka na pili kwa kuonyesha kuwa rais ameshindwa wa kufanya kazi.
Iwapo hoja ya kumshtaki Bungeni itapita katika Bunge la Kitaifa sheria ya kumshataki itapelekwa hadi kwa Seneti na ikiwa angalau thuluthi mbili ya maseneta wote watapiga kura kuunga mkono shtaka lolote la kumshtaki, Rais ataondolewa madarakani.
Kwa hali ilivyo sasa, Bunge linalopaswa kumshtaki Rais lilivunjwa Alhamisi Juni 9 2022.
Vile vile, Uhuru amebakiza wiki 8 tu kabla ya kumaliza muhula wake wa pili wa uongozi huku nchi ikipanga kumchagua Rais ajaye mnamo Agosti 9.