Search
Close this search box.
East Africa

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga kuelekea mahakamani

7
Kingozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga alipotoa hotuba yake kwa taifa baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.

Sasa ni wazi kuwa mgombea wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga atarejea katika mahakama ya upeo mwaka huu baada ya tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kumtangaza William Ruto kama mshindi wa uchaguzi mkuu wa agosti mwaka 2022.

Odinga amezungumza jumanne kwa mara ya kwanza tangu matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya IEBC Wafula Chebukati kupinga matokeo ambayo ameyataja kuwa si halali.

“Kile ambacho tuliona jana ni ukiukaji wa katiba na Wafula Chebukati. Mwenyekiti wa IEBC hana mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi iwapo nusu ya makamishna hawajakubaliana na matokeo hayo.” Alisema Odinga.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 77 ametaja matokeo hayo ya IEBC kuwa ya uwongo na  sasa ametangaza kuwa atakuwa akwenda katika mahakama ya upeo kupinga matokeo.

“Sitaki kuzungumzia sana kuhusu mipango yetu kuendelea mbele ila tutatumia njia zote za kikatiba na kisheria zilizoko” amesema Kinara huyo wa Azimio.

Kiongozi huyo ambaye amekuwa katika mrengo wa upinzani kwa muda mrefu, alipoteza nafsi yake ya tano ya kuingia ikulu dhidi ya naibu wa rais sasa William Ruto ambaye ametangazwa kuwa rais mteule siku ya jumatatu baada ya ngoja ngoja ya siku sita.

Wafuasi wa Odinga wamelalama kuibiwa kura katika kinyang’anyiro hicho jambo ambalo pia limezua mgawanyiko ndani ya tume ya kusimamia uchaguzi Kenya IEBC.

Odinga anasema Wafula Chebukati alisimamia zoezi hilo kwa njia ya kidikteta na kukiuka sheria alipoamua kutangaza matokeo hayo pasi na makamishna wanne kukubaliana naye.

“Sheria iko wazi kuhusu jukumu la mwenyekiti wa IEBC. Sheria haimpi mwenykiti nguvu za kuingoza IEBC kwa mabavu,” Odinga amesisitiza.

Makamishna wanne wa IEBC walijitenga na matokeo yaliotangazwa na mwenyekiti wao Wafula Chebukati kwa madai kuwa hakukuwa na uwazi katika shughuli ya mwisho ya ujumuishaji.

Kiongozi huyo wa upinzani amewataka wafuasi wake kuzingatia amani wakati wakiendelea kujadiliana kuhusu hatua hiyo ya kuelekea katika mahakama ya Upeo.

Katiba ya Kenya inatoa nafasi ya mwaniaji yeyote aliye na malalam kuhusu matokeo ya uchaguzi kuwasilisha kesi katika mahakama ya upeo siku saba baada ya mwenyekiti wa IEBC kuyatangaza.

Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa upinzani kuelekea mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu.

Mwaka wa 2013 aliwasilisha kesi baada ya rais wa sasa Uhuru Kenyatta kuibuka mshindi na jaji mkuu aliyestaafu Willy Mutunga akaitupilia mbali kwa kukosa ushahidi wa kutosa kuonyesha kuwa kulishuhudiwa wizi wa kura.

Mwaka wa 2017 vilevile Odinga alirejea mahakani kupinga kuchaguliwa kwa rais Kenyatta kwa muhula wake wa pili.

Mahakama ya upeo hata hivyo ilibatilisha matokeo hayo na kuitaka IEBC kurejelea zoezi la uchaguzi ambapo Odinga alijiondoa katika Kinyang’anyiro hicho.

Comments are closed

Related Posts